Kliniki katika kitovu cha Ebola nchini DR Congo 'yazidiwa' na wagonjwa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i138932-kliniki_katika_kitovu_cha_ebola_nchini_dr_congo_'yazidiwa'_na_wagonjwa
Ripoti zinasema kuwa, hospitali katika eneo lililoathiriwa na Ebola la Bunia katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imejaa idadi kubwa ya wagonjwa wa Ebola.
(last modified 2026-06-06T11:23:50+00:00 )
Jun 06, 2026 11:10 UTC
  • Kliniki katika kitovu cha Ebola nchini DR Congo 'yazidiwa' na wagonjwa

Ripoti zinasema kuwa, hospitali katika eneo lililoathiriwa na Ebola la Bunia katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imejaa idadi kubwa ya wagonjwa wa Ebola.

Kliniki ya Elikya ni mojawapo ya hospitali nyingi za eneo hilo inayoshuhudia ongezeko kubwa la wagonjwa kutokana na uhaba wa vifaa.

"Tumezidiwa kutokana na kuongezeka idadi ya wagonjwa, tuna wagonjwa wengi lakini hatuna pa kuwaweka. Tuko katika mchakato wa kujipanga na tunatumai kwamba baada ya muda mfupi kituo kitakuwa kinafanya kazi vizuri na tutaweza kushughulikia matatizo haya," amesema Yazid Yassin, mkurugenzi wa matibabu wa kliniki ya Elikya.

Mlipuko was Ebola umeathiri majimbo matatu ya mashariki mwa Congo DR, huku kitovu kikiwa Ituri, ambacho Africa CDC inasema kinachangia asilimia 90 ya visa vilivyothibitishwa vya Ebola na asilimia 76 ya vifo vilivyothibitishwa.

Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni za Shirika la Afya Duniani (WHO), kuna visa 381 vilivyothibitishwa nchini DRC, ikiwa ni pamoja na vifo 64 vilivyosababishwa na ugonjwa huo.

Mlipuko wa sasa wa Ebola ulitangazwa tarehe 15 Mei kaskazini mashariki mwa DRC. Hata hivyo, mamlaka za afya zinaamini kwamba aina ya Bundibugyo ya virusi vya Ebola, ambayo ni nadra sana, tayari ilikuwa imesambaa bila kugunduliwa kwa muda.

Ebola imeua zaidi ya watu 15,000 barani Afrika katika kipindi cha miaka 50 iliyopita. Mlipuko mbaya zaidi nchini DRC uliua karibu wagonjwa 2,300 kutoka kwenye kesi 3,500 za maambukizi ya virusi hivyo kati ya 2018 na 2020.