Askari wa UN waliwanajisi watoto CAR
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i1402-askari_wa_un_waliwanajisi_watoto_car
Askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wamekuwa wakiwadhalilisha kijinsia watoto wanne wanaoishi katika kambi ya wakimbizi huko Jamhuri ya Afrika ya Kati.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 17, 2016 03:36 UTC
  • Askari wa UN waliwanajisi watoto CAR

Askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wamekuwa wakiwadhalilisha kijinsia watoto wanne wanaoishi katika kambi ya wakimbizi huko Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Waathirika hao wanne walinajisiwa kati ya mwaka 2014 na 2015, amebaini msemaji wa Umoja wa Mataifa Farhan Haq.

Kikosi cha Kulinda amani cha Umoja wa Mataifa huko Jamhuri ya Afrika ya Kati MINUSCA kimekuwa kikumbwa na kashfa za askari wake kuwadhalilisha kingono watoto. Hii ni katika hali ambayo kikosi hicho kina jukumu la kuwalinda raia katika nchi hiyo inayokumbwa na ghasia.

Mbali na askari wa Kiafrika, askari wa Ulaya hasa wa Ufaransa pia wanatajwa kuhusika na vitendo hivyo visivyo vya kibinadamu dhidi ya watoto wadogo wa Jamhuri ya Afrika ya Kati ambao wanakabiliwa na hali mbaya ya kimaisha kutokana na nchi yao kukumbwa na machafuko ya umwagaji damu mkubwa tangu mwaka 2013.

Wananchi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati wamekuwa wakiandamana mara kwa mara kuonyesha kutoridhishwa kwao na utendaji wa kikosi hicho cha Umoja wa Mataifa pamoja na vitendo vyake vya ubakaji.

Katikati ya mwezi Agosti mwaka jana, wataalamu huru walisema Umoja wa Mataifa umefali vibaya katika kusimamia faili la kashfa za ngono jambo ambalo lilipelekea kufutwa kazi Babacar Gaye raia wa Senegal aliyekuwa kamanda wa MINUSCA.