UN yalaani kutumiwa mabavu dhidi ya raia Jamhuri ya Afrika ya Kati
Umoja wa Mataifa umelaani kuuliwa raia katika machafuko mapya ya makundi yenye silaha huko Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Kouassi Lazare Etien Mwakilishi wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa huko Jamhuri ya Afrika ya Kati amesema kuwa kitendo cha kushambuliwa raia nchini humo kinatia wasiwasi na kukwamisha usambazaji wa misaada ya kibinadamu nchini humo. Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kwamba, jambo la kusikitisha ni kuwa raia ndio wanaodhurika na mashambulizi na mapigano ya wanamgambo wenye silaha, baadhi yao huuawa na wengine wengi hulazimika kuyahama makazi yao.
Kouassi Lazare Etien ameongeza kuwa raia ambao wamelazimishwa kuwa wakimbizi huko Jamhuri ya Afrika ya Kati wanahitaji huduma za tiba, afya na chakula. Hata hivyo akasema kuwa kuendelea machafuko nchini humo kunakwamisha zoezi la kufikishwa kwa raia misaada ya kibinadamu. Machafuko mapya yaliyoikumba Jamhuri ya Afrika ya Kati yameshasababisha vifo vya watu 30 na kujeruhiwa wengine 50.