Mkapa azitaka pande husika Burundi kuheshimu mchakato wa amani
Rais Mstaafu wa Tanzania ambaye pia ni mpatanishi wa mgogoro wa Burundi amezitaka pande husika katika nchi hiyo kushikamana na kuheshimu mchakato wa amani na hatua zilizopigwa za kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa kisiasa wa nchi hiyo.
Rais mstaafu wa Tanzania, Benjamin Mkapa aliyasema hayo jana katika taarifa iliyotumwa kwa pande zinazoshiriki mchakato wa kuutafutia ufumbuzi mzozo huo na kuongeza kuwa, kuna haja kwa pande zote za kisiasa nchini Burundi kuheshimu juhudi zinazofanywa na Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC.
Mkapa ameongeza kuwa, tangu mwezi Mei mwaka huu hadi sasa, usalama umeimarika kwa kiasi fulani nchini Burundi kutokana na pande hasimu za kisiasa kuheshimu mchakato wa amani na kujiepusha na migogoro.
Rais Yoweri Museveni wa Uganda ambaye ni mpatanishi mkuu wa mgogoro wa Burundi anatazamiwa kukabidhiwa waraka wenye ramani ya njia ya kuelekea kwenye makubaliano ya kudumu hii leo Ijumaa. Yumkini mwafaka wa mwisho ukasainiwa na pande zote kufikia Juni mwaka ujao 2017.
Duru mpya ya mazungumzo ya kuutafitia ufumbuzi mzozo wa Burundi kwa kuwashirikisha wawakilishi kutoka EAC na viongozi wa serikali ya Burundi na wapinzani, ilianza tarehe 21 mwezi Mei mjini Arusha. Hata hivyo muungano mkuu wa wapinzani wa Burundi umekuwa ukisusia kushiriki kwenye mazungumzo hayo.
Machafuko na umwagaji damu ulianza kushuhudiwa nchini Burundi mwezi Aprili mwaka jana na kushtadi baada ya Rais wa nchi hiyo Pierre Nkurunziza kuamua kugombea urais kwa muhula wa tatu mfululizo, hatua ambayo wapinzani wanasema ni kinyume na katiba na makubaliano ya amani yaliyofikiwa Arusha, Tanzania.