Watoto 11 wafariki dunia katika ajali ya basi kaskazini mwa Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i21889-watoto_11_wafariki_dunia_katika_ajali_ya_basi_kaskazini_mwa_nigeria
Watoto 11 wamepoteza maisha baada ya kugongwa na basi walipokuwa wakishiriki zefe (matembezi) ya Maulid (kumbukumbu ya kuzaliwa Mtume SAW) kaskazini mwa Nigeria.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 21, 2016 23:35 UTC
  • Watoto 11 wafariki dunia katika ajali ya basi kaskazini mwa Nigeria

Watoto 11 wamepoteza maisha baada ya kugongwa na basi walipokuwa wakishiriki zefe (matembezi) ya Maulid (kumbukumbu ya kuzaliwa Mtume SAW) kaskazini mwa Nigeria.

Ahmed Usman, msemaji wa polisi ya Nigeria amesema ajali hiyo ilitokea Jumanne katika kijiji cha Malam Sidi, jimbo la Gombe, baada ya basi hilo kupoteza mwelekeo kutokana na kukatika breki na kuwagonga watoto hao waliokuwa wakishiriki matembezi hayo ya Maulidi.

Ramani ya Nigeria

Amesema watu wengine 17 wamejeruhiwa katika ajali hiyo na kuongeza kuwa, wahanga wa ajali hiyo ni watoto wa umri wa kati ya miaka 11 na 15.

Inaarifiwa kuwa, baada ya kutokea ajali hiyo, umati uliokuwa na ghadhabu ulimshambulia dereva wa basi hilo na kumpa kichapo hadi akafariki dunia huku polisi ikianzisha uchunguzi kuhusu ajali hiyo.

Nchi ya Nigeria imekuwa ikikumbwa na visa vya ajali za barabarani kutokana na hali mbaya za magari, barabara pamoja na kutozingatiwa sheria za barabarani.