Uchunguzi wa changamoto za bara la Afrika katika kikao cha Bamako
Kikao cha 27 cha viongozi wa nchi za Kiafrika na Ufaransa kimeanza leo Ijumaa huko Bamako mji mkuu wa Mali kwa shabaha ya kuchunguza masuala ya kiuchumi, migogoro ya Kisasa na kiusalama yanayolikabili bara la Afrika.
Kikao hicho ambacho kinawashirikisha zaidi ya viongozi 30 wa Kiafrika kitajadili na kuchunguza masuala mbalimbali yanayolihusu bara la Afrika ikiwemo migogoro ya kiusalama na masuala ya kidemokrasia na kiuchumi. Kikao hicho kinafanyika katika hali ambayo nchi nyingi za bara la Afrika zinakabiliwa na changamoto tofauti zikiwemo za hitilafu za ndani, vita na mapigano, njaa na ukame, uingiliaji wa kigeni na kutwishwa siasa za kikoloni. Katika hali ya hivi sasa wananchi wa nchi kama vile Sudan Kusini, Burundi, Gambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wanakumbwa na migogoro tofauti ya kisiasa. Nchini Gambia msimamo wa Rais Yahya Jammeh wa nchi hiyo wa kuendelea kungángánia madaraka licha ya kushindwa katika uchaguzi mkuu wa rais uliofanyika hivi karibuni, kila siku unaendelea kuisukuma nchi hiyo katika ukingo wa mgogoro mkubwa na hatari wa kisiasa. Nchini Burundi mazungumzo na Rais Pierre Nkurunziza wa nchi hiyo kwa ajili ya kuhitimisha mgogoro wa ndani hayajazaa matunda yoyote na hivyo kuruhusu kuendelea wimbi la mauaji ya kigaidi na mabavu katika nchi hiyo hiyo ndogo ya Kiafrika. Nchini Sudan Kusini mauji ya raia yamefikia kiwango cha kutajwa kuwa ni mauaji ya kizazi. Ni wazi kuwa migogoro hiyo ya kisiasa imevuruga usalama wa kieneo.
Katika upande wa pili kuongezeka kwa shughuli za makundi ya kigaidi katika nchi nyingi za Kiafrika kumebadilika na kuwa changamoto muhimu ya kieneo na kimataifa. Magharibi mwa bara hilo shughuli za kundi la kigaidi la Boko Haram na za as-Shabaab katika eneo la Mashariki zimevuruga kabisa usalama wa maeneo hayo. Kwa kutumia utajiri na nafasi za kijiografia za nchi kadhaa za bara hilo, makundi hayo ya kigaidi yamekuwa yakidumisha shughuli zao za kigaidi na hivyo kuvuruga utulivu na uthabiti wa nchi za eneo na hata kuzua wasiwasi wa kuenezwa shughuli hizo katika maeneo mengine ya dunia. Kuzuka kwa migogoro ya kisiasa na kiusalama, kumechochea pia migogoro ya kiuchumi katika nchi nyingi za Kiafrika.
Nyingi ya nchi hizo licha ya kuwa na utajiri mkubwa wa maliasili kama vile dhahabu, almasi na mafuta lakini zinakabiliwa na umasikini na ukosefu mkubwa wa ajira kutokana na kutokuwepo mipango madhubuti ya maendeleo, uwekezaji na teknolojia na kukumbwa na migogoro tofauti ya ndani. Hata kama hatua muhimu zimechukuliwa katika baadhi ya nchi kwa ajili ya kuboresha uchumi lakini mkondo huo wa maenedelo na marekebisho ya kiuchumi umeathirika pakubwa na hata kusimama katika baadhi ya sehemu kutokana na migogoro.
Katika upande wa pili, bara hilo limekuwa likitazamwa kwa jicho la tamaa na nchi koloni na hasa Ufaransa ambayo imejiimarisha katika nchi nyingi za bara hilo kwa ajili ya kupora utajiri wazo. Kikao cha Bbamako kinafanyika katika hali ambayo nchi nyingi za Kiafrika zinakabiliwa na matatizo makubwa ya kisiasa, kiuchumi na kiusalama, matatizo ambayo kwa hakika yamevuka mipaka na kuzitishia hata nchi za Ulaya zenyewe.
Kwa msingi huo inaonekana kuwa huu ni wakati muwafaka wa kufanyika vikao kama hivyo ili kujaribu kutatua matatizo yanayozikabili pande mbili za Afrika na Ulaya, na hasa yale yanayohusiana na uchumi na usalama. Pamoja na hayo ni wazi kuwa vikao kama hivyo vitafanikiwa tu pale nchi koloni za Magharibi zitakapoacha kikamilifu kufuatilia malengo yao ya siri na ya kikoloni katika nchi za Afrika na kwa upade wa pili viongozi wa nchi za Kiafrika watakapoachana kabisa na tabia yao mbovu ya kukandamiza demokrasia na kuamua kufuatilia malengo ya kudhamini maslahi ya kitaifa na ya kieneo ya bara la Afrika.