11 wauawa Nigeria kwa kushiriki maandamano ya kumuunga mkono Trump
Wanachama 11 wa harakati ya Biafra nchini Nigeria wanaripotiwa kuuawa na maafisa usalama katika maandamano yaliyofanyika kusini mashariki mwa nchi.
Habari zinasema kuwa, maafisa usalama wa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika waliwakabili wanaharakati wa Biafra katika mji bandari wa Harcourt, walipokuwa wakifanya maandamano na mijumuiko ya kuashiria uungaji mkono wao kwa Rais mpya wa Marekani Donald Trump ambaye aliapishwa jana. Aidha wanachama zaidi ya 100 wa vuguvugu hilo la Biafra wamekamatwa katika maandamano na mikusanyiko hiyo ya jana.
Prince Emmanuel Kanu, ndugu ya kiongozi wa harakati hiyo ambaye yuko kizuizini tangu Oktoba 2015, Nnamdi Kanu, amesema waliamua kufanya maandamano hayo kwa kuwa harakati hiyo inaunga mkono sera na misimamo ya Trump, kama vile kupigania jambo kwa ukakamavu na bila kukata tamaa.
Itakumbukwa kuwa, shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International mwishoni mwa mwaka uliopita wa 2016 lilisema wanaharakati wapatao 150 wa vuguvugu hilo linaloshinikiza kujitenga na Nigeria waliuawa na jeshi la nchi hiyo kati ya Agosti mwaka juzi 2015 na Agosti mwaka jana, wakishiriki maandamano ya amani.
Aidha Disemba mwaka jana, Mahakama Kuu ya Nigeria ilikataa kumuachia huru kwa dhamana mkuu wa harakati ya Biafra inayopigania kujitenga na Nigeria. Jaji wa Mahakama Kuu ya Federali mjini Abuja Binta Nyako alisema, tuhuma zinazomuandama Nnamdi Kanu, mkuu wa harakati ya kupigania kujitenga na Nigeria eneo la Biafra la kusini mwa nchi hiyo ni nzito na kwa msingi huo hawezi kupewa dhamana.