Watu 12 wafariki dunia kwenye mgodi nchini Msumbiji
Kwa akali watu 12 wamepoteza maisha baada ya mgodi kuwaporomokea katika mkoa wa Zambézia nchini Msumbiji.
Shirika la habari la DW limeripoti kuwa, mbali na maafa hayo, wachimba mgodi wengine kadhaa wamejeruhiwa katika ajali hiyo iliyofanyika katika kijiji cha Muiane wilaya ya Gilé.
Almeida Manhiça, Mkurugenzi wa Maliasili katika mkoa wa Zambézia nchini Msumbiji amesema kuwa, ajali za kuporomoka kwa migodi zimeongezeka mno nchini katika siku za hivi karibuni hususan katika eneo hilo.
Mgodi huo wa madini ya tantalite katika wilaya ya Gile umekosa usimamizi mzuri baada ya shirika moja la Canada kulitelekeza miezi kadhaa iliyopita.
Mara kwa mara serikali ya Maputo imekuwa ikiwakataza watu kuchimba migodi iwapo hawajaidhinishwa na vyombo husika. Aghalabu ya wanaojihusisha na kazi hiyo ya kuchimba migodi nchini humo hawana suhula zinazohitajika, vibali wala kuidhinishwa na vyombo vya dola.
Msumbiji iliyoko kusini mashariki mwa Afrika, ina watu milioni 24 na inahesabiwa kuwa moja ya nchi maskini zaidi duniani, licha ya kuwa na utajiri mkubwa wa madini na gasi asilia.