Njaa yawanyemelea maelfu Nigeria kutokana na ugaidi wa Boko Haram
(last modified Thu, 09 Feb 2017 04:06:43 GMT )
Feb 09, 2017 04:06 UTC
  • Njaa yawanyemelea maelfu Nigeria kutokana na ugaidi wa Boko Haram

Maelfu ya watu wanakabiliwa na hatari ya baa la njaa nchini Nigeria kutokana na mashambulizi ya kundi la kigaidi la Boko Haram.

Ripoti iliyotolewa leo na Umoja wa Mataifa imesema kuwa, baa la njaa linahatarisha maisha ya maelfu ya watu wa Nigeria kutokana na mashambulizi ya kundi hilo la kigaidi.

Ripoti hiyo imesema kuwa, asilimia 65 ya wakazi wa jimbo la Borno huko kaskazini mwa Nigeria ambako ndiko yaliko makao makuu ya Boko Haram wanakabiliwa na hatari ya baa la njaa. Imeongeza kuwa, kwa ujumla watu milioni 11 wa Nigeria watasumbuliwa na uhaba wa chakula katika mwaka huu wa 2017.

Njaa na utapiamlo Nigeria

Wakati huo huo Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) limetangaza kuwa, mgogoro mkubwa zaidi wa kibinadamu barani Afrika utashadidi zaidi huko kaskazini mashariki mwa Nigeria katika kipindi cha uhaba wa chakula yaani baina ya miezi ya Juni na Agosti.

Mashambulizi yanayoendelea kufanywa na kundi la kigaidi la Boko Haram katika maeneo hayo yamewalazimisha mamilioni ya watu kukimbia makazi yao na kukwamisha shughuli za kilimo.