Watu wasiopungua 30 wauawa Kasai nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i24993-watu_wasiopungua_30_wauawa_kasai_nchini_jamhuri_ya_kidemokrasia_ya_congo
Watu wasiopungua 30 wameuawa katika mji wa Tshimbulu Kasai Katikati huko katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kufuatia mashambulio ya kundi moja la wanamgambo.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Feb 11, 2017 04:00 UTC
  • Watu wasiopungua 30 wauawa Kasai nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo

Watu wasiopungua 30 wameuawa katika mji wa Tshimbulu Kasai Katikati huko katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kufuatia mashambulio ya kundi moja la wanamgambo.

Vyombo vya usalama vya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo vimetangaza kuwa,  watu 30 wameuawa katika shambulio la wanamgambo dhidi ya mji wa Tshimbulu  huko Kasai ya Kati.

Taarifa za awali zinasema kuwa, wanamgambo wanaomuunga mkono Kamuina Nsapu kiongozi wa zamani wa kundi hilo ndio waliotekeleza shambulio hilo katika mji wa Tshimbulu. 

Makumi ya watu pia wanaripotiwa kujeruhiwa katika shambulio hilo. Mwezi Januari uliopita, wanamgambo hao walifanya shambulio jingine kama hilo katika mji huo na kupelekea watu kadhaa kuuawa.

Waasi wa ADF Nalu

Kamuina Nsapu aliuawa mwaka jana na vikosi vya usalama vya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Tangu wakati huo, miji kadhaa na vijiji vya mji wa Kasai ya Kati na Kasai ya Mashariki imekuwa ikishuhudiwa vurugu, machafuko na mapigano kati ya vikosi vya usalama na wanamgambo hao wanaomuunga mkono kiongozi wao wa zamani Kamuina Nsapu.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, maeneo ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo yamekuwa yakishuhudia machafuko kwa zaidi ya miongo miwili sasa na yanahesabiwa kuwa ngome ya makundi ya waasi yanayoendesha harakati zao katika nchi hiyo yakiwemo makundi ya waasi kutoka nje ya nchi hiyo kama LRA, FDLR na ADF-Nalu.