Ethiopia yakataa wito wa UN na EU wa kufanyika uchunguzi dhidi yake
Waziri Mkuu wa Ethiopia amekataa wito wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya wa kufanyika uchunguzi huru juu ya mauaji ya mamia ya watu wakati wa maandamano ya miezi kadhaa dhidi ya serikali ya Addis Ababa nchini humo.
Hailemariam Desalegn amesema Ethiopia ina uwezo wa kuchunguza mauaji hayo na kusisitiza kuwa serikali yake haitaruhusu wachunguzi wa kimataifa kuingia nchini humo kwa ajili ya kadhia hiyo.
Waziri Mkuu wa Ethiopia amewaambia waandishi wa habari mjini Addis Ababa kuwa Tume ya Kitaifa ya Haki za Binadamu tayari inachunguza mauaji hayo na kwamba matokeo ya uchunguzi huo yatawekwa wazi karibuni hivi.
Agosti mwaka jana, Zeid Raad al-Hussein, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa aliitaka Ethiopia kushirikiana na umoja huo katika kuchunguza vifo hivyo vya mamia ya watu wanaodaiwa kuuawa na vyombo vya dola kwa kushiriki maandamano dhidi ya serikali, wito ambao uliungwa mkono na Umoja wa Ulaya mapema mwezi huu.
Mwishoni mwa mwezi uliopita, Bunge la Ethiopia lilitangaza habari ya kurefushwa sheria ya hali ya hatari nchini humo kwa muda wa miezi minne zaidi, wiki mbili baada ya serikali kufuta sheria hiyo.
Zaidi ya watu elfu 11 wamekamatwa nchini Ethiopia tangu Oktoba mwaka jana, kwa kukiuka sheria ya hali ya hatari iliyotangazwa mapema mwezi huo, kufuatia mivutano ya kisiasa na malalamiko ya upinzani wa wananchi yaliyoshuhudiwa katika miji kadhaa nchini humo miezi kadhaa kabla ya hapo.