May 01, 2017 13:50 UTC
  • Wanajeshi kadhaa wa Nigeria wauawa katika shambulio la wanamgambo wa Boko Haram

Kundi la kigaidi la Boko Haram limefanya shambulio katika kambi moja ya jeshi la Nigeria na kuwaua wanajeshi kadhaa wa nchi hiyo.

Ripoti zaidi kutoka Nigeria zinasema kuwa, kwa akali wanajeshi wanane wameuawa kufuatia shambulio la wanamgambo wa Boko Haram dhidi ya kambi moja ya jeshi katika mji wa Damboa ulioko katika jimbo la Borno. 

Ripoti ya jeshi inasema kuwa, wanajeshi kadhaa wamejeruhiwa pia katika shambulio la wanamgambo hao ambao wamehatarisha amani na usalama katika maeneo ya kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Jeshi la Nigeria limeanzisha uchunguzi juu ya kiwango cha shambulio hilo ambalo limezusha hofu na wasiwasi miongoni mwa raia walioko jirani na kambi hiyo ya jeshi.

Wanachama wa Boko Haram

Kundi la Boko Haram lilianzisha mashambulizi dhidi ya maeneo ya umma na taasisi za serikali huko kaskazkini mwa Nigeria mwaka 2009 na baadaye mwaka 2015 likapanua mashambulizi hayo hadi katika nchi za Chad, Cameroon na Niger.

Zaidi ya watu elfu 20 wameuwa hadi sasa katika mashambulizi hayo na mamilioni ya wengine wamelazimika kuwa wakimbizi.

Serikali ya Rais Muhamadu Buhari inakosolewa vikali kwa kushindwa kukabiliana na kundi la Boko Haram. Hata kikosi cha pamoja cha nchi za eneo kilichoundwa kwa shabaha ya kukabiliana na wanamgambo hao wa Boko Haram kinaonekana kushindwa kufikia malengo yake. 

Tags