Rais Buhari wa Nigeria arejea London, Uingereza kwa matibabu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i28800-rais_buhari_wa_nigeria_arejea_london_uingereza_kwa_matibabu
Muda mfupi baada ya kuonana na wanafunzi wa kike 82 waliokuwa wamewatekwa nyara na kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram katika mji wa Chibok mwaka 2014, mkabala wa kuachiwa huru wafungwa wa kundi hilo, Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria ameondoka nchini na kwenda Uingereza kwa ajili ya kile kinachosemwa ni uchunguzi wa kiafya.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 08, 2017 02:23 UTC
  • Rais Buhari wa Nigeria arejea London, Uingereza kwa matibabu

Muda mfupi baada ya kuonana na wanafunzi wa kike 82 waliokuwa wamewatekwa nyara na kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram katika mji wa Chibok mwaka 2014, mkabala wa kuachiwa huru wafungwa wa kundi hilo, Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria ameondoka nchini na kwenda Uingereza kwa ajili ya kile kinachosemwa ni uchunguzi wa kiafya.

Taarifa ya Ikulu ya Rais imesema kuwa: Hakuna haja ya kuwa na wasiwasi, madaktari wake mjini London ndio watakaoamua atasalia nchini Uingereza kwa muda gani kwa ajili ya matibabu.

Jumatano iliyopita, Rais Buhari kwa mara nyingine tena alishindwa kuhudhuria kikao cha baraza la mawaziri kwa sababu za kiafya, hiyo ikiwa ni mara ya tatu kwa kiongozi huyo wa taifa kushindwa kuhudhuria kikao hicho kutokana na kuendelea kusumbuliwa na maradhi.

Buhari na wasichana wa Shule ya Upili ya Chibok waliaochiwa huru na Boko Haram

Hii ni katika hali ambayo, serikali na familia ya Buhari haijaweka wazi kuhusu ugonjwa unaomsumbua rais huyo wa Nigeria mwenye umri wa miaka 74. 

Siku chache zilizopita, kundi moja la wanaharakati nchini Nigeria lilimtaka Rais Buhari kuchukua likizo ya matibabu kufuatia wasiwasi kuhusu hali yake ya kiafya huku baadhi ya wanaharakati wakimtaka ajiuzulu.

Itakumbukwa kuwa, mwezi Machi mwaka huu, Buhari alirejea nchini Nigeria akitokea mjini London nchini Uingereza ambako alikuwa likizo kwa muda wa siku 51 kwa ajili ya matibabu.