Rais Kabila atangaza serikali ya mpito, akipuuza chama kikuu cha upinzani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i28880-rais_kabila_atangaza_serikali_ya_mpito_akipuuza_chama_kikuu_cha_upinzani
Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ametangaza serikali mpya ya mpito licha ya makelele ya wapinzani wanaosema amekiuka makubaliano ya pande mbili.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
May 09, 2017 23:52 UTC
  • Rais Kabila atangaza serikali ya mpito, akipuuza chama kikuu cha upinzani

Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ametangaza serikali mpya ya mpito licha ya makelele ya wapinzani wanaosema amekiuka makubaliano ya pande mbili.

Asilimia kubwa ya mawaziri na manaibu waziri 60 wanaounda serikali ya mpito ya Kongo DR iliyotangazwa jana Jumanne wamewahi kuhudumu katika serikali iliyopita, huku wizara nyeti kama vile ya Mambo ya Nje, Mambo ya Ndani, Sheria na Madini zikikabidhiwa wapambe wa Rais Kabila.

Mwezi uliopita, Rais Kabila alimteua Bruno Tshibala mmoja wa viongozi wa upinzani kuwa Waziri Mkuu, ikiwa ni katika kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa Disemba 31 mwaka jana kati ya wapinzani na serikali ya Kongo ili kuiondoa nchi hiyo katika mgogoro wa kisiasa.

Bruno Tshibala, Waziri Mkuu wa DRC

Hata hivyo viongozi wa chama kikuu cha upinzani cha Union for Democracy and Social Progress (UDPS) hawakuridhia uteuzi huo wakisisitiza kuwa, Felix Tshisekedi mwana wa kiume wa marehemu mzee Etienne Tshisekedi mwanasiasa mkongwe wa nchi hiyo ndiye alikuwa chaguo lao. 

Joseph Kabila ambaye aliingia madarakani mwaka 2001 baada ya kuuliwa baba yake Laurent Desire Kabila, alishinda katika chaguzi mbili za mwaka 2006 na 2011. Kwa mujibu wa katiba, duru ya uongozi wa Kabila ilipasa kumalizika mwezi Disemba mwaka jana, ambapo asingeweza kugombea kiti cha urais kwa muhula mwingine wa tatu.

Hata hivyo kwa mujibu wa makubaliano hayo ya Disemba mwaka jana ambayo chama cha UPDS kinasema hayana itibari tena, Kabila aliruhusiwa kuendelea kubakia uongozini hadi mwishoni mwa mwaka huu wa 2017.