Watu 14 wauawa katika mashambulio ya Boko Haram nchini Nigeria
Jeshi la polisi la Nigeria limetangaza kuwa, magaidi wa genge la Boko Haram wamefanya mashambulizi katika mji wa Maiduguri, makao makuu ya jimbo la Borno la kaskazini mwa nchi hiyo na kuua watu 14.
Shirika la habari la Reuters limenukuu Damian Chukwu, mkuu wa jeshi la polisi katika jimbo la Borno akitangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, jana usiku magaidi wa Boko Haram waliushambulia mji wa Maiduguri kwa kutumia silaha za kujikinga na mashambulizi ya anga. Mji wa Maiduguri umekuwa kituo cha mashambulizi ya kigaidi wa Boko Haram tangu mwaka 2009.
Hivi sasa kundi hilo la kigaidi limeshadidisha mashambulizi yake dhidi ya raia na maafisa wa kulinda usalama wa Nigeria.
Tangu lilipoanzisha mashambulizi yake nchini Nigeria mwaka 2009 hadi hivi sasa, genge hilo limeshauwa watu wasiopungua 20 elfu na kuwafanya wakimbizi zaidi ya watu milioni mbili na laki sita wengine. Mamia ya maelfu ya watu wamejeruhiwa kwenye mashambulizi ya Boko Haram, kundi ambalo hivi sasa limepanua maeneo ya mashambulizi yake ni kuzijumuisha nchi nne jirani za Nigeria, Niger, Chad na Cameroon.
Wakati wa kampeni za uchaguzi, ilani kuu ya Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria ilikuwa ni kuliangamiza kundi hilo mara atakapoingia madarakani. Hata hivyo si tu rais huyo wa nigeria ameshindwa kutimiza ahadi zake kwa wananchi, lakini pia ameelekeza nguvu zake katika kuwakandamiza Waislamu wengine wasiofanya vitendo vya kigaidi na hadi hivi sasa serikali yake inaendelea kukaidi amri ya Mahakama Kuu ya Nigeria ya kumwachilia huru Sheikh Ibrahim Zakzaky, mkuu wa Jumuiya ya Kiislamu ya Nigeria aliyepigwa risasi na kujeruhiwa vibaya wakati jeshi la nchi hiyo lilipokuwa linawakandamiza Waislamu huko Zaria.