Kwa akali watu 16 wauawa katika shambulio la kujiripua, kaskazini mwa Nigeria
Habari kutoka Nigeria zinaarifu kwamba, kwa akali watu 16 wameuawa na wengine 11 kujeruhiwa, katika mashambulizi kadhaa ya kujiripua kwa mabomu katika jimbo la Borno, kaskazini mashariki mwa Nigeria.
Polisi ya jimbo la Borno limetangaza kuwa, mashambulizi hayo ya kigaidi yametekelezwa na wanawake watano katika mji wa Maiduguri, makao makuu ya jimbo hilo la Borno. Kwa kawaida mashambulizi kama hayo hufanywa na wanachama wa kundi la kigaidi na ukufurishaji la Boko Haram.
Tarehe saba mwezi huu, wanachama wa kundi hilo walitekeleza hujuma kadhaa za kigaidi kupitia utegaji mabomu katika mji wa Maiduguri na kuua watu 14.
Hivi sasa wanachama wa kundi hilo ambalo mwaka 2015 lilitangaza utiifu wake kwa kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh, wamezidisha hujuma ndani na nje ya Nigeria. Kwa mujibu wa ripoti rasmi, katika kipindi cha miaka minane ya mashambulizi ya wanachama wa kundi hilo hadi sasa, kwa akali watu elfu 20 wameuawa na zaidi ya wengine milioni mbili na laki sita kuwa wakimbizi.