Rais wa Nigeria ajaribu kutuliza malumbano ya kikabila
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i30882-rais_wa_nigeria_ajaribu_kutuliza_malumbano_ya_kikabila
Kaimu Rais wa Nigeria, Profesa Yemi Osinbajo amekutana na viongozi wa maeneo kadhaa kujaribu kuzima malumbano ya kikabila yanayotokota katika nchi hiyo.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Jun 23, 2017 23:16 UTC
  • Rais wa Nigeria ajaribu kutuliza malumbano ya kikabila

Kaimu Rais wa Nigeria, Profesa Yemi Osinbajo amekutana na viongozi wa maeneo kadhaa kujaribu kuzima malumbano ya kikabila yanayotokota katika nchi hiyo.

Siku za hivi karibuni zimeshuhudia kuongezeka machafuko baina ya wakazi wa kaskazini mwa Nigeria wa kabila la Hausa na wale wa kusini mashariki wa kabila la Igbo.

Makundi hayo mawili yamekuwa yakirushiana lawama tokea mwanzo wa mwezi huu huku makabila ya Kaskazini mwa Nigeria yanayowajumuisha Wafulani, Wahausa na Waberom wakitaka Waigbo watimuliwe kaskazini mwa nchi hiyo kwa sababu ya harakati zao za uasi wa kutaka kujitenga na kuunda taifa lao la Biafra kusini mashariki mwa nchi.

Matakwa ya kutaka Waigbo watimuliwe yanakumbusha yaliyojiri miaka 51 iliyopita nchini humo wakati kundi hilo lilipoanzisha vita vya kutaka kujitenga Biafra mwaka 1967. Vita hivyo vilimalizika kwa ushindi wa Jeshi la Nigeria mwaka 1970 huku watu milioni moja wakifariki.

Kaimu Rais Osinbajo amewatahadharisha viongozi wa pande zote mbili kuhusu chuki za kikabila na kusema ni hatari kwa umoja wa nchi hiyo.