Senegal yaonya kuhusu hatari za kupinduliwa serikali ya Gambia
Waziri wa Mambo ya Nje wa Senegal ameonya kuwa ukosefu wa utulivu na machafuko yanatishia uwepo wa serikali mpya ya Gambia.
Mankeur Ndiaye alisema hayo jana na sambamba na kuonya kuhusiana na ukubwa na hatari zinazoikabili serikali mpya ya Gambia amesema kuwa, nchi yake itaendelea kuunga mkono juhudi za Rais Adama Barrow ya kufanyia marekebisho mfumo wa kiulinzi na kiusalama wa Gambia.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Senegal amesema kuwa nchi yake haitoruhusu machafuko na ukosefu wa amani urejee nchini Gambia.
Yahya Jammeh, rais wa zamani wa Gambia aliiongoza kidikteta nchi hiyo ndogo ya magharibi mwa Afrika kwa muda wa miaka 22 hadi alipopalizika kukimbilia nchini Guinea Conakry tarehe 21 Januari mwaka huu baada ya kushadidi mgogoro wa kisiasa na kiusalama nchini mwake uliotokana na kukataa kwake kuondoka madarakani baada ya kushindwa katika uchaguzi.
Uchaguzi wa Rais wa Gambia ulifanyika mwezi Disemba mwaka jana na Adama Barrow alishinda katika uchaguzi huo.
Rais wa wakati huo wa Gambia, Yahya Jammeh awali alikubali kushindwa lakini ghafla moja alibadilisha msimamo wake na kudai kuwa kumefanyika udanganyifu katika uchaguzi huo. Hata hivyo nchi jirani na Gambia na za magharibi mwa Afrika hususan Senegal zilimlazimisha Yahya Jammeh aondoke madarakani kupenda asipende.