Watu 19 wauawa katika hujuma ya kigaidi Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i31672-watu_19_wauawa_katika_hujuma_ya_kigaidi_nigeria
Watu 19 wamepoteza maisha na wengine wengi kujeruhiwa kufuatilia milipuko kadhaa ya mabomu iliyotokea kaskazini mashariki mwa Nigeria.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 12, 2017 09:58 UTC
  • Watu 19 wauawa katika hujuma ya kigaidi Nigeria

Watu 19 wamepoteza maisha na wengine wengi kujeruhiwa kufuatilia milipuko kadhaa ya mabomu iliyotokea kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Polisi wamesema Jumatano ya leo kuwa mashambulizi hayo yalijiri Jumanne usiku katika mji wa Maiduguri ambao ni makao makuu ya jimbo la Borno ambalo ni ngome ya magaidi wakufurishaji wa Boko Haram.

Kamishna wa Polisi wa Borno, Damian Chukwu amesema watu 12 waliouawa walikuwa wanachama wa Kundi la Raia Wanaojihami, na watu wengine saba walishambuliwa na magaidi punde baada ya kufika eneo la tukio.

Danbatte Bello, msemaji wa Kundi la Raia Wanojihami amesema moja kati ya magaidi waliojifunga mishipi ya mabomu na kujilipua alikuwa mwanamke. Amesema magaidi hao walikuwa wanawalenga kwa makusudi wanamgambo wa Kundi la Raia Wanaojihami ambao walikuwa wakilinda doria.

Hakuna kundi lolote lililodai kuhusika na hujuma hiyo lakini inashabihiana sana na mashambulizi ambayo hutekelezwa na magaidi wa Kiwahabi wa kundi la Boko Haram.

Tangu lianzishe uasi wake mwaka 2009, kundi la Boko Haram limeua raia zaidi ya 20,000 huku wengine milioni mbili wakilazimika kuacha makazi yao nchini Nigeria, na pia nchi jirani za Cameroon, Chad na Niger.

Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa, ugaidi wa Boko Haram umewafanya watu milioni 4.5 wahitajie misaada ya chakuka kutokana na kuvurugika shughuli za kilimo.