Upinzani Zimbabwe wajiweka sawa ili kumbwaga Mugabe 2018
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i32770-upinzani_zimbabwe_wajiweka_sawa_ili_kumbwaga_mugabe_2018
Kinara wa upinzani nchini Zimbabwe, Morgan Tsvangirai ametangaza kuungana na wapambe wake wa zamani kwa shabaha ya kuunda muungano mmoja wenye nguvu ili waweze kumundoa madarakani Rais Robert Mugabe katika uchaguzi mkuu mwakani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 06, 2017 02:34 UTC
  • Upinzani Zimbabwe wajiweka sawa ili kumbwaga Mugabe 2018

Kinara wa upinzani nchini Zimbabwe, Morgan Tsvangirai ametangaza kuungana na wapambe wake wa zamani kwa shabaha ya kuunda muungano mmoja wenye nguvu ili waweze kumundoa madarakani Rais Robert Mugabe katika uchaguzi mkuu mwakani.

Tsvangirai ambaye ni kiongozi wa chama cha upinzani cha MDC amesema ameamua kuungana na kushirikiana na manaibu wake wawili waliokuwa pamoja katika serikali tete iliyopita ya mseto kuanzia mwaka 2009 hadi 2013.

Miongoni mwa shakhsia watakaounda muungano mpya wa upinzani kwa ajili ya kuchuana na chama tawala ZANU-PF chake Mugabe ni Naibu Waziri Mkuu wa zamani katika serikali ya mseto Welshman Ncube na mpambe wake wa karibu Tendai Biti.

Kadhalika veterani Agrippa Mutambara, mkuu wa chama cha Zimbabwe People First amejiunga na muungano huo wa upinzani.

Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe

Mwezi Aprili mwaka huu, Tsvangirai alisema yeye na Joyce Mujuru, ambaye alikuwa Makamu wa Rais wa Mugabe hadi alipotimuliwa mwaka 2014, watapigania kuunda serikali ya mseto ili kuleta mabadiliko ya kisiasa nchini humo; hata hivyo haijabainika iwapo msimamo huo ungalipo. 

Chama tawala nchini Zimbabwe ZANU-PF ambacho kinaiongoza nchi hiyo tangu ipate uhuru wake mwaka 1980, mwezi Desemba mwaka jana kilimpitisha rasmi Mugabe kuwa mgombea wake wa urais katika uchaguzi unaotazamiwa kufanyika katikati ya mwaka ujao ambapo kiongozi huyo atakuwa ametimiza umri wa miaka 94.