Watu wasiopungua 12 wauawa katika shambulio dhidi ya kanisa Nigeria
Watu wasiopungua 12 wameuawa kusini mashariki mwa Nigeria na makumi ya wengine kujeruhiwa baada ya watu waliokuwa na silaha kuvamia kanisa moja na kuanza kuwamiminia watu risasi.
Taarifa zaidi zinasema kuwa, kanisa katoliki la St. Philip la mji wa Ozubulu katika jimbo la Anambra ndilo lililolengwa na shambulio hilo ambapo washambuliaji waliwamimia ovyo risasi waumini waliokuwa ndani ya kanisa hilo.
Baadhi zinasema kuwa, hakuna takwimu rasmi za idadi ya watu waliouawa na kwamba, inawezekana idadi ya waliouawa katika shambulio hilo la kigaidi ikawa zaidi ya iliyotangazwa.
Aidha kuna majeruhi wengi wa shambulio hilo ambao wanaendelea kupata matibabu hospitalini huku hali za baadhi yao zikiripotiwa kuwa mbaya.
Baadhi ya duru zinasema kuwa, waliotekeleza shambulio hilo walikuwa watu watano wenye silaha ambao walikuwa wamefunika nyuso zao.
Inasadikiwa kuwa, huenda waliotekeleza shambulio hilo wakawa ni wanachama wa kundi la kigaidi la Boko Haram.
Tangu lilipoanzisha mashambulizi yake nchini Nigeria mwaka 2009 hadi hivi sasa, genge hilo limeshaua watu wasiopungua 20 elfu na kuwafanya wakimbizi zaidi ya watu milioni mbili na laki sita.
Serikali ya Rais Muhamadu Buhari inakosolewa vikali kwa kushindwa kukabiliana na kundi la Boko Haram. Hata kikosi cha pamoja cha nchi za eneo kilichoundwa kwa shabaha ya kukabiliana na wanamgambo hao wa Boko Haram kinaonekana kushindwa kufikia malengo yake.