Rais Buhari wa Nigeria kutowania muhula wa pili mwaka 2019
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i34031-rais_buhari_wa_nigeria_kutowania_muhula_wa_pili_mwaka_2019
Waziri mmoja wa ngazi za juu nchini Nigeria amesema Rais Muhamadu Buhari wa nchi hiyo hatagombea muhula wa pili katika kinyang'anyiro cha urais kinachotazamiwa kufanyika mwaka 2019.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 07, 2017 09:36 UTC
  • Rais Buhari wa Nigeria kutowania muhula wa pili mwaka 2019

Waziri mmoja wa ngazi za juu nchini Nigeria amesema Rais Muhamadu Buhari wa nchi hiyo hatagombea muhula wa pili katika kinyang'anyiro cha urais kinachotazamiwa kufanyika mwaka 2019.

Aisha Alhassan, Waziri wa Masuala ya Wanawake wa Nigeria ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, mwaka 2014/2015 Buhari aliahidi kuwa atagombea muhula mmoja tu kwa lengo la 'kusafisha kero na changamoto' zilizosababishwa na serikali iliyopita ya PDP na kwamba hatagombea muhula wa pili.

Waziri huyo amesema iwapo Buhari atawania muhula wa pili kinyume na ahadi yake, basi atajiengua madarakani sambamba na kumuunga mkono makamu wa rais wa zamani wa nchi hiyo Atiku Abubakar iwapo ataamua kugombea kiti hicho.

Rais Buhari akirejea nchini kutoka London

Hata hivyo wasemaji wawili wa Rais Buhari wamekataa kulizungumzia suala hilo la iwapo ni rasmi Buhari hatowania muhula wa pili au la.

Mwishoni mwa mwezi uliopita, Rais Muhamadu Buhari wa Nigeria alirejea nyumbani, baada ya kuwa nje ya nchi kwa miezi mitatu akipata matibabu katika mji mkuu wa Uingereza London.

Buhari alilazimika kurejea nchini baada ya wananchi wa Nigeria kufanya maandamano makubwa wakitaka ima arejee nyumbani au ajiuzulu.