Odinga: Wafuasi wetu wasiandamane siku ya uchaguzi wa marudio
Kinara wa muungano wa upinzani NASA nchini Kenya amewataka wafuasi wa mrengo huo kutofanya maandamano wakati wa uchaguzi wa marudio wa urais unaotazamiwa kufanyika Alkhamisi wiki hii.
Katika mahojiano na shirika la habari la BBC, Raila Odinga amesema: "Sisi hatujawaambia wafuasi wetu waandamane siku ya uchaguzi. Tumewataka wabakie majumbani mwao."
Hii ni katika hali ambayo, hivi karibuni Odinga alinukuliwa na vyombo vya habari akiitisha maandamano makubwa siku ya Alkhamisi, akisisitiza kuwa hakuna uchaguzi utafanyika iwapo masharti yao hayatatekelezwa.
Polisi wametumia mabomu ya gesi ya kutoa machozi kuzima maandamano ya wafuasi wa NASA mjini Kisumu na katika mji mkuu Nairobi hii leo.
Huku hayo yakiarifiwa, Kaimu Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kenya Fred Matiang'i amesema kesho Jumatano na Alkhamisi, Oktoba 26 zitakuwa siku za mapumziko ili kutoa fursa kwa wananchi wanaotaka kupiga kura kusafiri kwenda kwenye maeneo walikojisajili.
Katika hatua nyingine, Hakimu Chacha Mwita wa Mahakama Kuu ametupilia mbali ombi la kuitaka mahakama hiyo imlazimishe Odinga kushiriki uchaguzi huo wa marudio.
Mahakama ya Juu ya Kenya ilibatilisha uchaguzi wa Agosti 8 baada ya Odinga kuwasilisha kesi ya kupinga ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta wa chama cha Jubilee na kuagiza kufanyika uchaguzi mpya ndani ya siku 60.