AU: Ulaya unahusika katika matatizo yanayolikumba bara la Afrika
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i36719-au_ulaya_unahusika_katika_matatizo_yanayolikumba_bara_la_afrika
Mwenyekiti wa hivi sasa wa Umoja wa Afrika, Rais Alpha Condé wa Guinea Conakry amesema kuwa, Umoja wa Ulaya unahusika katika sehemu ya matatizo yanayolikabili bara la Afrika.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 24, 2017 00:49 UTC
  • Rais Alpha Condé wa Guinea Conakry
    Rais Alpha Condé wa Guinea Conakry

Mwenyekiti wa hivi sasa wa Umoja wa Afrika, Rais Alpha Condé wa Guinea Conakry amesema kuwa, Umoja wa Ulaya unahusika katika sehemu ya matatizo yanayolikabili bara la Afrika.

Rais Condé amesema hayo Alkhamisi katika mazungumzo na waandishi wa habari aliyoyafanya kwa pamoja na Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa mjini Paris na kusisitiza kuwa, Ulaya ni sehemu ya matatizo ya Afrika hasa suala la wahajiri wanaokufa maji katika fukwe za Libya na magendo ya binadamu nchini humo. Amesema, Libya haina uwezo wa kuhudumia wimbi kubwa la wahajiri linaloingia nchini humo.

Kabla ya hapo Umoja wa Ulaya ulikuwa umeitaka Libya itafute misaada ya kifedha ya kuzuia kumiminika wahajiri na wakimbizi nchini humo kuelekea barani Ulaya.

waki

Wakimbizi wakijaribu kuingia barani Ulaya kupitia Libya

 

Fayez al Sarraj, waziri mkuu wa serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya hivi karibuni alifichua kuwa, Umoja wa Ulaya umekataa kutekeleza ahadi zake za kuisaidia nchi hiyo kukabiliana na wimbi la wakimbizi.

Wiki iliyopita, baadhi ya vyombo vya habari vilitangaza habari ya kupigwa mnada na kuuzwa kama watumwa wahajiri wa Kiafrika nchini Libya kwa dola 400 kila mmoja. Suala hilo limezikasirisha sana nchi za eneo hilo pamoja na taasisi za kieneo na kimataifa.

Wimbi kubwa sana la wakimbizi huko Libya ni matunda ya uingiliaji wa madola ya Magharibi hususan katika eneo la Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika ambalo limekuwa mzigo pia kwa nchi hizo za Magharibi.