Somalia yasema hatua ya Trump dhidi ya Quds ni 'hatari'
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i37409-somalia_yasema_hatua_ya_trump_dhidi_ya_quds_ni_'hatari'
Somalia imejiunga na nchi nyingine za Afrika kulaani hatua ya Rais wa Marekani, Donald Trump ya kuitangaza Baytul Muqaddas kuwa mji mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 10, 2017 00:10 UTC
  • Somalia yasema hatua ya Trump dhidi ya Quds ni 'hatari'

Somalia imejiunga na nchi nyingine za Afrika kulaani hatua ya Rais wa Marekani, Donald Trump ya kuitangaza Baytul Muqaddas kuwa mji mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel.

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Somalia imeutaja uamuzi huo wa Trump kama 'hatari' huku ikiitaka serikali ya Washington kuuangalia upya na kutafakari kuhusu athari zake.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, kitendo hicho cha Trump kitakuwa na taathira hasi sio tu kwa eneo la Mashariki ya Kati, bali kote duniani; huku ikizitaka nchi za Kiislamu na Kiarabu kuchukua hatua za kivitendo za kuihami Palestina.

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Somalia imebainisha kuwa, serikali na taifa la Mogadishu liko tayari kutetea haki za Wapalestina kwa hali na mali.

Ramani ya Somalia

Viongozi wa nchi nyingi za Afrika zikiwemo Misri, Tunisia, Algeria, Tanzania, Morocco na Kenya wamekosoa vikali hatua hiyo ya kichokozi ya Trump.

Kadhalika Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki Mahamat sanjari na kulaani hatua hiyo ya Trump, amebainisha kwamba, uamuzi wa Rais wa Marekani utazidisha hali ya wasiwasi katika eneo la Mashariki ya Kati na kwamba umoja huo unatilia mkazo na kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Wapalestina za kutaka kuunda dola lao huru la Palestina mji mkuu wake ukiwaBaitul Muqaddas.