ICC yazijia juu nchi wanachama kwa kutomkamata Rais wa Sudan
Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) amezikosoa vikali baadhi ya nchi wanachama wa Mkataba wa Roma uliounda mahakama hiyo, kwa kukataa kumtia mbaroni Rais Omar al-Bashir wa Sudan alipozitembelea.
Fatou Bensouda amesema kitendo hicho cha baadhi ya nchi wanachama kama vile Uganda, Jordan na Chad kinaidhalilisha na kuipotezea hadhi makahama hiyo iliyoko mjini The Hague nchini Uholanzi.
Kadhalika Bensouda amelishutumu Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, akisema kuwa limeshindwa kuchukua hatua dhidi ya Bashir na shakhsia wengine wanaoandamwa na tuhuma za kufanya jinai dhidi ya binadamu na jinai za kivita katika eneo la Darfur huko magharibi mwa Sudan tangu mwaka 2003.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lina mamlaka ya kuiwekea vikwazo nchi yoyote mwanachama inayokataa kushirikiana na Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai.
Bashir aliitembelea Uganda katikati ya mwezi uliopita wa Novemba, huku Chad ikimpokea Rais huyo wa Sudan wiki ya kwanza ya mwezi Disemba. Kabla ya hapo, Omar al-Bashir aliizuru Jordan mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu.
Maelfu ya watu wameuawa na mamilioni ya wengine kulazimika kuwa wakimbizi kutokana na mauaji na machafuko yanayoendelea katika jimbo la Darfur huko magharibi mwa Sudan.