Rais wa Zimbabwe: Nitaheshimu matokeo ya uchaguzi wa rais
Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe ameahidi kuwa nchi hiyo itafanya uchaguzi wa urais kabla ya Julai mwaka huu na kwamba ataheshimu uamuzi wa wananchi.
Mnangagwa ameyasema hayo leo Jumatano katika Mkutano wa Kimataifa wa Uchumi mjini Davos nchini Uswisi na kusisitiza kuwa, binafsi hana uchu wa madaraka na ataachia ngazi iwapo atabwagwa na upinzani katika uchaguzi huo.
Kadhalika ameuambia mkutano huo kuwa, serikali yake licha ya kumpa mtangulizi wake Robert Mugabe kitita kikubwa cha pensheni na posho nyingine, lakini rais huyo wa zamani wa Zimbabwe hajapewa kinga ya kutoshtakiwa.
Hivi karibuni Mnangagwa ambaye alishika wadhifa wa urais wa Zimbabwe mwezi uliopita baada ya jeshi na chama tawala Zanu-Pf kumshinikiza Robert Mugabe aliyekuweko madarakani kwa muda kwa miaka 37 ajiuzulu alinukuliwa na vyombo vya habari akitangaza kwamba, nchi hiyo itaitisha uchaguzi mkuu katika kipindi cha miezi minne hadi mitano ijayo, na kwamba atagombea kiti hicho kupitia chama tawala Zanu-Pf.
Siku chache zilizopita, Roy Bennett, kiongozi wa upinzani aliyekuwa akiishi uhamishoni alifariki dunia katika ajali ya helikopta iliyotokea katika jimbo la New Mexico nchini Marekani.