Nigeria inaendelea kumzuilia Sheikh Zakzaky kwa amri ya Marekani
Mwanaharakati wa kisiasa nchini Nigeria amekosoa vikali hatua ya serikali ya Abuja ya kukataa kumuachia huru mwanachuoni mashuhuri wa Kiislamu, Sheikh Ibrahim Zakzaky licha ya agizo la mahakama, na kusisitiza kuwa msomi huyo anaendelea kuzuiliwa kwa amri ya Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Katika mahiojiano na shirika la habari la Tasnim, Yusuf Hamza amesema serikali ya Nigeria ilipokea agizo la kumkamata na kumzuilia mwanaharakati huyo wa Kiislamu pamoja na mkewe kutoka kwa watawala wa Washington na Tel Aviv na hadi sasa wanaendelea kuzuiliwa katika mazingira magumu ya kuogofya licha ya hali yao ya kiafya kuwa mbaya.
Hii ni katika hali ambayo, wanachama wa Harakati ya Kiislamu nchini Nigeria wanaendeleza maandamano ya amani ya kutaka aachiliwe huru kiongozi wao Sheikh Ibrahim Zakzaky.
Taarifa zinasema kuwa mwishoni mwa wiki hii maandamano yameendelea katika maeneo mbali mbali ya Nigeria hasa katika mji wa Zaria jimboni kaduna ambapo waandamanaji wametaka Sheikh Zazkay na mke wake waachiliwe huru mara moja.
Itakumbukwa kuwa, Sheikh Ibrahim Zakzaky alitiwa nguvuni na jeshi la Nigeria mwezi Disemba mwaka 2015 baada ya kuvamia makazi yake katika mji wa Zaria jimboni Kaduna na kufanya mauaji ya umati dhidi ya Waislamu.
Taarifa zinasema mamia ya Waislamu waliuawa shahidi katika hujuma hiyo wakiwemo watoto watatu wa Sheikh Zakzaky.