Makumi ya magaidi wa Boko Haram wauawa Nigeria
Makumi ya wapiganaji wa kundi la kigaidi la Boko Haram wameuawa nchini Nigeria.
Msemaji wa Jeshi la Nigeria, Kanali Sani Othman amesema kuwa, magaidi 25 wa kundi la Boko Haram wameangamizwa katika operesheni ya jeshi hilo iliyofanyika katika maeneo ya vijijini kwenye jimbo la Borno. Kanali Othman ameongeza kuwa, jeshi la Niger limeendeleza operesheni ya kuwafagia magaidi wa Boko Haram katika vijiji vitatu vya Borno na kuteka aina mbalimbali za silaha na zana za vita. Ameongeza kuwa raia 18 wakiwemo watoto wadogo 9 waliokuwa wakishikiliwa mateka na kundi hilo la kigaidi pia wamekombolewa.
Maelfu ya watu wameuawa na mamilioni ya wengine kulazimika kukimbia makazi yao nchini Nigeria kufuatia mashambulizi yanayofanywa na kundi la kigaidi la Boko Haram hususan katika maeneo ya kaskazini mwa nchi hiyo. Kundi hilo pia limepanua zaidi ukatili na mashambulizi yake katika nchi jirani kama Chad na Cameroon.