Mufti wa Tanzania azitaka taasisi za Hija zimuogope Mwenyezi Mungu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i42310-mufti_wa_tanzania_azitaka_taasisi_za_hija_zimuogope_mwenyezi_mungu
Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakary Zubeir amezitaka taasisi zote zinazojihusisha na usafirishaji wa mahujaji, kufanya shughuli zao kwa utaratibu unaostahili, huku wakimuogopa Mwenyezi Mungu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 28, 2018 03:37 UTC
  • Mufti wa Tanzania azitaka taasisi za Hija zimuogope Mwenyezi Mungu

Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakary Zubeir amezitaka taasisi zote zinazojihusisha na usafirishaji wa mahujaji, kufanya shughuli zao kwa utaratibu unaostahili, huku wakimuogopa Mwenyezi Mungu.

Mufti Zubeir ametoa nasaha hizo jijini Dar es Salaam wakati alipokuwa akizindua kampeni maalumu chini ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), yenye lengo la kuwahamasisha waumini wa dini ya Kiislamu kwenda kutekeleza ibada ya Hija.

Mufti Mkuu wa Tanzania amesema kuwa, ibada ya Hija ni moja kati ya maagizo muhimu ndani ya dini ya Kiislam inayomtaka kila muumini mwenye uwezo kwenda kuitekeleza, lakini inashangaza kuona baadhi ya taasisi zinavyoshindwa kulisimamia suala hilo kikamilifu kwa kuwatendea waumini mambo yasiyostahili.

Amesema: “Tumeshuhudia huko nyuma baadhi ya viongozi wa taasisi wamekuwa wakali kwa waumini wao bila ya kujua madhara yake, hili si jambo zuri, wanapaswa kufanya shughuli hii kwa ajili ya Mwenyezi Mungu wakitambua kuwa waumini ni kama wanafunzi wanaopaswa kuelimishwa,”.

Baadhi ya Waislamu waliowahi kukwamba katika Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam walipokuwa wakitaka kuuelekea kufanya ibada ya Hija

Mufti Zubeir ameongeza kuwa,  viongozi wa taasisi hizo pamoja na waumini wao wanapaswa kuwa na mshikamano utakaosaidia kudumisha misingi ya dini hiyo, huku akiwasisitizia viongozi hao kufanya kazi ya ziada ili kuepuka kukosa radhi za Mtume Muhammad (SAW).

Wakati huo huo, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Bakwata Taifa, Sheikh Hamisi Mataka, amezitaka taasisi zote zinazothibitishwa katika usafirishaji wa mahujaji mwaka huu, kuhakikisha wanatimiza matakwa yaliyowekwa ili kuepusha matatizo yaliyowahi kujitokeza siku za nyuma.

Aidha amezitaka taasisi hizo kuhakikisha zimewasilisha nyaraka muhimu, zikiwemo za taratibu, malipo na riba kwa ajili ya safari ya Mahujaji hao kabla ya Aprili 10, mwaka huu, hatua aliyosema kuwa itasaidia kuondoa hofu ya mahujaji hao kushindwa kusafiri.