Rais wa Ghana: Hatutairuhusu Marekani ijenge kituo cha kijeshi nchini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i42740-rais_wa_ghana_hatutairuhusu_marekani_ijenge_kituo_cha_kijeshi_nchini
Rais Nana Akufo-Addo wa Ghana amesema nchi hiyo katu haitasaini mkataba na Marekani wa kuiruhusu Washington ijenge kituo cha kijeshi katika nchi hiyo ya Kiafrika.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 06, 2018 23:22 UTC
  • Rais wa Ghana: Hatutairuhusu Marekani ijenge kituo cha kijeshi nchini

Rais Nana Akufo-Addo wa Ghana amesema nchi hiyo katu haitasaini mkataba na Marekani wa kuiruhusu Washington ijenge kituo cha kijeshi katika nchi hiyo ya Kiafrika.

Akihutubia taifa kwa njia ya televisheni, Rais wa Ghana amesema, "Siwezi kuwa rais ambaye atakuwa tayari kuuza uhuru wa kujitawala nchi yake. Ninaheshimu kumbukumbu ya wapigania uhuru wa taifa hili, ambao walijitoa muhanga ili nchi hii iwe huru."

Hata hivyo amesisitiza kuwa, nchi hiyo inaweza kusaini mkataba wa kuimarisha uhusiano wa kiulinzi na Marekani, lakini kamwe haiwezi kuiruhusu nchi hiyo ijenge vituo vyake vya kijeshi ndani ya nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Jumatano ya wiki iliyopita, maelfu ya wananchi wa Ghana waliandamana katika mji mkuu Accra kupinga mkataba tata wa kijeshi baina ya nchi yao na Marekani.

Wananchi wa Ghana wakiandamana dhidi ya kujengwa kambi za kijeshi za US nchini humo

Rais wa zamani wa Ghana John Dramani Mahama wa chama cha upinzani cha NDC amesema anapinga vikali mapatano hayo baina ya serikali ya nchi yake na Marekani.

Katika miezi ya hivi karibuni Marekani imekuwa ikijaribu kuimarisha satwa yake ya kijeshi katika nchi kadhaa za Kiafrika kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi.