Wanajeshi wa Israel wawapiga wanawake wa Kipalesatina na kuwavua hijabu zao
(last modified Thu, 05 Jul 2018 07:52:04 GMT )
Jul 05, 2018 07:52 UTC
  • Wanajeshi wa Israel wawapiga wanawake wa Kipalesatina na kuwavua hijabu zao

Wanajeshi wa Israel wametenda jinai nyingine baada ya kuwapiga, kuwadhalilisha na kuwavua hijabu wanawake wa Kipalestina katika kijiji cha Khan al-Ahmar mashariki mwa mji wa Quds.

Tukio hilo lilitokea wakati wanajeshi wa utawala haramu wa Israel walipowasili katika eneo hilo wakiambatana na mabuldoza wakiwa tayari kubomoa nyumba za Wapalestina katika kijiji hichjo ambapo Wapalestina walijitokeza na kukabiliana na wanajeshi hao.

Baada ya vurugu hizo, wanajeshi wa Israel waliwatia mbaroni wanawake kadhaa wa Kipalestina ambapo waliwapiga na kuwadhalilisha na kisha kuwavua hijabu zao.  

Kitendo hicho cha kuwapiga, kuwadhalisha na kuwavua hijabu wanawake wa Kipalestina kimelaaniwa mno na Wapalestina na asasi mbalimbali.

Maandamano ya Wapalestina ya "Haki ya Kurejea".

Wakati huo huo, Hilali Nyekundu ya Palestina imetangaza kuwa, Wapalestina 35 wamejeruhiwa katika kijiji hicho cha Khan al-Ahmar wakati walipokuwa wakiwazuia wanajeshi wa Israel wasibomoe nyumba zao.

Hujuma hizo za Israel zinakwenda sambamba na kushadidi maandamano ya Haki ya Kurejea wakimbizi wa Kipalestina yaliyoanza tangu Machi mwaka huu na ambayo yamewatia kiwewe viongozi wa utawala huo ghasibu.

Inaeelezwa kuwa, idadi ya Wapalestina waliouawa shahidi katika maandamano ya "Haki ya Kurejea" tangu yalipoanza tarehe 30 Machi mwaka huu imefikia 144 huku wengine wasiopungua 15,501 wakiwa wamejeruhiwa.

Madola ya Magharibi ikiwemo Marekani, yameendelea kulaaniwa na walimwengu kutokana na kuendelea kuunga mkono na kuusadia utawala huo ghasibu wa Israel.

Tags