Dakta Mukwege wa Kongo DR ashinda Tuzo ya Amani ya Nobel
(last modified Fri, 05 Oct 2018 15:44:25 GMT )
Oct 05, 2018 15:44 UTC
  • Dakta Mukwege wa Kongo DR ashinda Tuzo ya Amani ya Nobel

Denis Mukwege, daktari bingwa wa upasuaji raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo pamoja na mwanaharakati wa Iraq, Nadia Murad wametangazwa washindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel kwa mwaka huu 2018.

Kamati ya Nobel nchini Norway imesema kuwa, wanaharakati hao wametunukiwa tuzo hiyo kwa pamoja kutokana na jitihada zao za kupambana na unyanyasaji wa kingono kama silaha ya vita.

Dakta Mukwege ambaye ni tabibu wa magonjwa ya wanawake anaripotiwa kujitolea kuwatibu na kuwasaidia wanawake ambao ni wahanga wa jinai za kingono nchini Kongo DR; huku Nadia Murad, ambaye ni mmoja wa wanawake 3,000 wa Kiyazidi wahanga wa jinai za kingono za kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS) nchini Iraq, akituzwa kwa kufichua na kuzungumzia jinai hizo.

Tuzo ya Amani ya Nobel ya mwaka jana wa 2017 ilitunukiwa kundi la kimataifa linaloendesha kampeni ya kupigwa marufuku silaha za nyuklia duniani la iCAN. 

Tuzo ya Amani ya Nobel

Shakhsia wengine wa bara la Afrika ambao wamewahi kutunukiwa tuzo hiyo ya kifahari ni pamoja na aliyekuwa kiongozi wa vita dhidi ya ubaguzi wa rangi (apartheid) nchini Afrika Kusini hayati Nelson Mandela, aliyeibuka baadaye kuwa rais wa kwanza aliyechaguliwa kidemokrasia nchini humo na Dakta Kofi Annan, aliyekuwa Katibu Mkuu wa UN, ambaye aliaga dunia hivi karibuni na kuzikwa katika nchi yake ya Ghana.

Wengine ni Askofu Desmond Tutu wa Afrika Kusini ambaye amewahi kuwa Katibu Mkuu wa Baraza la Makanisa ya Afrika Kusini, aliyekuwa rais wa Liberia, Ellen Johnson Sirleaf na Mkenya marehemu Wangari Maathai, aliyekuwa mtetezi wa mazingira na mwanzilishi wa shirika la Green Belt Movement.  

Tags