HRW yataka kushtakiwa askari wanaowakandamiza Waislamu Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i50120-hrw_yataka_kushtakiwa_askari_wanaowakandamiza_waislamu_nigeria
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limetoa mwito wa kufunguliwa mashitaka wanajeshi wa Nigeria wanaowakandamiza Waislamu wa madhehebu ya Shia.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Dec 12, 2018 09:10 UTC
  • HRW yataka kushtakiwa askari wanaowakandamiza Waislamu Nigeria

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limetoa mwito wa kufunguliwa mashitaka wanajeshi wa Nigeria wanaowakandamiza Waislamu wa madhehebu ya Shia.

Aniete Ewang, Mtafiti wa Human Rights Watch nchini Nigeria ametoa mwito huu leo Jumatano na kuongeza kuwa, kuendelea wimbi la unyanyasaji, ukandamizaji na kushambuliwa Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini humo hakutakua na matokeo mengine ghairi ya kuvuruga zaidi hali ya usalama wa taifa nchini humo.

Amesema shirika hilo linatoa mwito wa kufikishwa mbele ya sheria maafisa wote usalama waliohusika katika ukandamizaji huo, wakiwemo wale wanaowashambulia mara kwa mara wafuasi wa mwanaharakati wa Kiislamu Sheikh Ibrahim Zakzaky, kila wanapoandamana kushinikiza kuachiwa huru kiongozi wao huyo.

Mwezi Oktoba mwaka huu, shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International lilithibitisha kuwa, Waislamu zaidi ya 45 waliuawa mjini Abuja katika mashambulizi yaliyofanywa na askari usalama wa Nigeria dhidi ya matembezi ya kidini ya wafuasi wa madhehebu ya Shia, wakati wa maadhimisho ya Ashura ya Imam Hussein AS.  

Sheikh Zakzaky kabla na baada ya kushambulia na askari wa Nigeria Disemba 2015

Disemba mwaka 2015, jeshi la Nigeria liliua kwa umati karibu wafuasi 1000 wa Sheikh Ibrahim Zakzaky wakiwemo wanawe watatu na baadaye kuwazika katika makaburi ya umati. 

Kadhalika idadi kubwa ya wafuasi wa Sheikh Ibrahim Zakzaky walikamatwa wakati jeshi na vikosi vya ulinzi vya Nigeria vilipofanya jinai na ukandamizaji mkubwa dhidi ya ofisi za Harakati ya Kiislamu ya Nigeria (IMN).