Muungano mkuu wa upinzani nchini Sudan wamtaka Rais Bashir ajiuzulu
Muungano mkubwa zaidi wa upinzani wa Nidaa nchini Sudan umemtaka Rais Omar al-Bashir wa nchi hiyo aachie ngazi, huku maandamano dhidi ya serikali yakiendelea.
Muungano wa upinzani wa Nidaa unaojumuisha Chama cha Umma kinachoongozwa na Waziri Mkuu wa zamani, Saddiq al-Mahdi na makundi ya kisiasa ya magharibi mwa Kordofan, maeneo ya Darfur na eneo la Blue Nile kusini mwa Khartoum ulitoa taarifa hiyo jana Jumatano, inayomtaka al Bashir ajiuzulu na kuanza kipindi cha mpito kuelekea kwenye demokrasia.
Katika hatua nyingine, vyombo vya dola nchini Sudan vimefunga intaneti na mitandao ya kijamii, ili kudhibiti maandamano hayo ya wananchi ya karibu wiki mbili sasa.
Wananchi wa Sudan wamekuwa wakifanya maandamano katika majimbo karibu yote ya nchi hiyo wakilalamikia hali mbaya ya uchumi na ughali wa bidhaa.
Maandamano hayo yaliyopewa jina la "Maandamano ya Mkate" sasa yamechukua mkondo mpya na waandamanaji wanataka kuondolewa madarakani serikali ya Rais Omar al Bashir.
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limeripoti kuwa, watu wasiopungua 38 wameuliwa hadi sasa katika machafuko hayo, huku serikali ikishikilia kuwa ni watu 19 pekee.