AU na UN zafufua mazungumzo ya amani Jamhuri ya Afrika ya Kati
Maafisa wa ngazi za juu wa Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa wako katika Jamhuri ya Afrika ya Kati kwa lengo la kuhuisha mchakato wa mazungumzo ya amani uliokwama tangu Julai mwaka 2017.
Taarifa ya Umoja wa Mataifa imesema kuwa, mbali na wawakilishi wa UN na AU, wajumbe kutoka Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Katikati mwa Afrika (ECCAS) pia watashirikishwa kwenye mazungumzo hayo ya amani.
Taarifa hiyo ya UN imeongeza kuwa, wajumbe wa jumuiya hizo za kikanda na kimataifa wanatazamiwa kuwaleta kwenye meza ya mazungumzo wawakilishi wa serikali na makundi ya watu wanaobeba silaha huko Jamhuri ya Afrika ya Kati, ili kuanzisha tena mazungumzo ambayo yataupatia ufumbuzi wa kudumu mgogoro huo unaoikabili nchi hiyo kwa miaka mingi sasa.
Miongoni mwa maafisa wa ngazi za juu wanaoshiriki mazungumzo haya yanayotazamiwa kuendelea hadi Alkhamisi ya kesho ni Jean-Pierre Lacroix, Naibu Katibu Mkuu wa UN anayeshughulikia operesheni za vikosi vya kulinda amani na Kamishna wa Masuala ya Amani wa AU, Smail Chergui.
Machafuko nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati yaliibuka mwaka 2013 baada ya wapiganaji wa Seleka kumuondoa madarakani aliyekuwa rais wa taifa hilo, François Bozizé; huku mgogoro ukishadidi baada ya wanamgambo wa Kikristo wenye misimamo ya kufurutu ada wa Anti-Balaka kuanzisha mauaji ya kutisha dhidi ya jamii ya Waislamu wa nchi hiyo.
Mbali na maelfu ya watu kuuawa na kujeruhiwa, makumi ya maelfu ya wengine wamelazimika kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi.