Zimbabwe yatumia wanajeshi kuzima maandamano, kadhaa wauawa
(last modified Tue, 15 Jan 2019 14:38:13 GMT )
Jan 15, 2019 14:38 UTC
  • Zimbabwe yatumia wanajeshi kuzima maandamano, kadhaa wauawa

Watu wasiopungua watano wameuawa na maafisa usalama huku maandamano ya kupinga ongezeko la bei ya mafuta kwa asilimia 150 nchini Zimbabwe yakishtadi.

Serikali imetumia wanajeshi kukabiliana na waandamanaji hii leo katika mji mkuu Harare na mji wa Bulawayo kusini mwa nchi, ambapo helikopta ya kijeshi imetumika kuwarushia waandamanaji hao mabomu ya gesi ya kutoa machozi.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu nchini humo yamesema kuwa, watu 26 wana majeraha ya risasi, na kwamba polisi imewatia mbaroni waandamanaji zaidi ya 200.

Maandamano hayo yameendelea kushuhudiwa licha ya Waziri wa Leba nchini humo,  Sekai Nzenza kusema kuwa serikali itawapa wafanyakazi wa umma nyongeza ya marupupu kwa asilimia 5 hadi 23, huku mazungumzo kati ya maafisa wa serikali na miungano ya wafanyakazi kuhusu nyongeza ya mishahara ikiendelea.

Walimu nchini Zimbabwe wakifanya maandamano mjini Harare

Haya yanajiri katika hali ambayo, watumishi wa umma nchini Zimbabwe kupitia miungano na vyama vya kutetea maslahi yao, Alkhamisi iliyopita walikataa nyongeza ya asilimia 10 ya mshahara iliyotangazwa na serikali.

 Walimu na madaktari nchini humo wapo katika mgomo kwa muda mrefu sasa wakisisitiza kuwa wanataka kulipwa mishahara yao kwa kutumia sarafu ya dola ya Marekani.

 

Tags