Viongozi wa Kiislamu Kenya: Ugaidi hauna dini wala kabila
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i50926-viongozi_wa_kiislamu_kenya_ugaidi_hauna_dini_wala_kabila
Viongozi wa Waislamu nchini Kenya wamelaani shambulizi la kigaidi la hivi karibuni katika mji mkuu Nairobi, lililopelekea kuuawa makumi ya watu, huku wakisisitiza kuwa ugaidi hauna dini wala kabila.
(last modified 2026-03-17T04:36:21+00:00 )
Jan 16, 2019 23:47 UTC
  • Viongozi wa Kiislamu Kenya: Ugaidi hauna dini wala kabila

Viongozi wa Waislamu nchini Kenya wamelaani shambulizi la kigaidi la hivi karibuni katika mji mkuu Nairobi, lililopelekea kuuawa makumi ya watu, huku wakisisitiza kuwa ugaidi hauna dini wala kabila.

Katika taarifa iliyosomwa jana katika Msikiti wa Jamia jijini Nairobi na Hassan Ole Naado, Naibu Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu nchini humo Supkem, kwa niaba ya baraza hilo na Baraza la Maimamu na Wahubiri nchini humo CIPK na Jukwaa la Viongozi wa Kiislamu Namlef, viongozi hao wa Kiislamu sambamba na kuzifariji familia za wahanga wa shambulio hilo, wamewataka Wakenya kutoingia katika mtego wa kufarakanishwa katika misingi ya dini na magenge ya kigaidi.

Taarifa hiyo imesisitiza kuwa, kitendo hicho cha kigaidi ni jambo lisilokubalika na ambalo linakiuka misingi yote ya thamani za utu na ubinadamu.

Wakati huohuo, Mkuu wa Polisi nchini humo, Inspekta Jenerali Joseph Boinnet amesema idadi ya wahanga wa hujuma hiyo imeongezeka na kufikia watu 21. Awali serikali ya Kenya ilitangaza kuwa waliopoteza maisha katika shambulio hilo la juzi Jumanne ni watu 15.

Aidha magaidi wote waliuawa na maafisa usalama wa Kenya katika shambulizi hilo la kigaidi na utekaji nyara uliodumu kwa muda wa masaa 19 katika Hoteli ya Dusit jijini Nairobi.

Mripuko wa mabomu nje ya Hoteli ya Dusit jijini Nairobi

Kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab lenye makao yake nchini Somalia limetangaza kupitia radio yake ya kipropaganda ya Andalus kuwa limehusika na shambulizi hilo.

Shambulizi hilo lilitokea mita chache kutoka Jengo la Westgate ambalo lilishambuliwa na wanachama wa al-Shabaab mwaka 2013, ambapo watu 67 waliuawa, na pia lilifanyika katika siku ya kumbukumbu ya shambulio la kundi la hilo la kigaidi na kitakfiri dhidi ya kambi ya kijeshi ya El-Adde, ambayo ilikuwa na askari wa Kenya KDF nchini Somalia, ambapo zaidi ya wanajeshi 100 wa Kenya waliuawa.