Tunisia yaungana na Lebanon na Iraq kutaka Syria irejeshwe Arab League
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i51145-tunisia_yaungana_na_lebanon_na_iraq_kutaka_syria_irejeshwe_arab_league
Waziri wa Mambo ya Nje wa Tunisia Khemaies Jhinaoui ametoa mwito kwa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kuirejeshea Syria kiti chake cha uwanachama katika jumuiya hiyo na kusisitiza kwamba "mahali pa kimaumbile" pa nchi hiyo ni katika jumuiya hiyo yenye nchi 22 wanachama.
(last modified 2026-03-03T12:46:59+00:00 )
Jan 27, 2019 04:09 UTC
  • Tunisia yaungana na Lebanon na Iraq kutaka Syria irejeshwe Arab League

Waziri wa Mambo ya Nje wa Tunisia Khemaies Jhinaoui ametoa mwito kwa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kuirejeshea Syria kiti chake cha uwanachama katika jumuiya hiyo na kusisitiza kwamba "mahali pa kimaumbile" pa nchi hiyo ni katika jumuiya hiyo yenye nchi 22 wanachama.

Akizungumza katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari aliofanya na waziri mwenzake wa Russia Sergei Lavrov, mjini Tunis hapo jana, Waziri wa Mambo ya Nje wa Tunisia alisema, Syria ni nchi ya Kiarabu, na mahali pake pa kipaumbile ni ndani ya Arab League.

Khamis Al-Jihinawi ameongeza kuwa, suala la Syria kurejea kwenye Jumuiya ya Nchi za Kiarabu halitegemei Tunisia, bali linategemea uamuzi wa jumuiya hiyo, na kwamba mwaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama ndio watakaotoa uamuzi juu ya kadhia hiyo.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Sergei Lavrov, naye pia ametoa mwito wa kutaka Syria irejeshewe uwanachama wake katika Arab League.

Al-Jihinawi (kulia) na Lavrov katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari

Mnamo tarehe 18 Januari, Waziri wa Mambo ya Nje wa Lebanon, Gebran Bassil aliitaka Jumuiya ya Nchi za Kiarabu iirejeshee Syria uwanachama wake katika jumuiya hiyo na kueleza kwamba, ni "kosa la kihistoria" kujaribu kuzuia hatua hiyo.

Mbali na Waziri wa Mambo ya Nje wa Lebanon, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq Muhammad al-Hakim, naye pia amesema nchi yake inaunga mkono kurejeshwa Syria katika Arab League.

Suala la uwezekano wa Syria kurejeshewa kiti chake cha uwanachama katika Jumuiya ya Nchi za Kiarabu linazungumziwa, hasa baada ya hatua ya hivi karibuni ya baadhi ya nchi za Kiarabu, ikiwemo Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Bahrain kufungua tena balozi zao mjini Damascus.../