Serikali ya Sudan yawakamata viongozi wa upinzani
Maafisa wa polisi nchini Sudan wamewatia mbaroni viongozi waandamizi wa vyama vya upinzani, muda mfupi kabla ya kuanza wimbi jipya la maandamano dhidi ya serikali.
Chama cha Congress cha Sudan kimetangaza kuwa, vinara kumi wa vyama mashuhuri vya upinzani nchini humo wamekamatwa hii leo kabla ya kuanza maandamano mapya katika mji mkuu Khartoum.
Kwa mujibu wa Sudanese Congress Party, miongoni mwa viongozi wa upinzani waliotiwa mbaroni ni Naibu Mwenyekiti wa chama cha Umma, Mariam Sadiq al-Mahdi; Katibu Mkuu wa chama hicho Sara Naqdallah na kinara wa Chama cha Kikomunisti Mokhtar al-Khatib, pamoja na wengine.
Kadhalika maafisa usalama nchini humo wamefyatua mabomu ya gesi ya kutoa machozi kutawanya mikusanyiko ya mamia ya watu waliokuwa wanapanga kuandamana dhidi ya serikali ya Rais Omar al-Bashir, karibu na Soko la Arab mjini Khartoum.
Chama cha Umma ambacho ni chama kikubwa zaidi cha upinzani nchini Sudan, kimetoa radiamali yake kuhusiana na vitisho vya serikali juu ya kutumia nguvu kali katika kukabiliana na waandamanaji na kusema kwamba serikali ya Rais Omar al-Bashir inataka kuanzisha wimbi jipya la mauaji nchini humo.
Katika hali ambayo viongozi wa serikali ya Khartoum wametangaza kwamba hadi sasa ni watu 30 pekee wamepoteza maisha katika ghasia hizo, lakini mashirika huru likiwemo shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International yanasema kwamba watu waliouawa kufikia sasa ni 57.