Ujenzi wa bomba la mafuta la Uganda, Tanzania yaipiku Kenya
Uganda imeamua kujenga bomba la mafuta kupitia Tanzania badala ya Kenya.
Hayo yamesemwa na maafisa wa Kenya waliohudhuria mkutano wa kujadili suala hilo.
Maafisa hao walisema wakiwa Kampala kwamba Uganda ilikataa kuungana na Kenya kujenga bomba la mafuta kutoka Hoima hadi Lamu kupitia Lokichar.
“Tumepoteza na sasa Uganda itapitishia mafuta yake Tanzania. Kilichobaki sasa ni kutafuta mbinu za kujenga bomba letu hadi bandari ya Lamu,” amesema afisa wa Kenya aliyehudhuria mkutano huo.
Yaliyojadiliwa katika mkutano huo hayakuwekwa wazi lakini waliohudhuria wanasema uamuzi wa mwisho utatangazwa kwenye mkutano wa marais wa nchi husika wiki ijayo.
Kulingana na The East African, huenda Uganda ilikubaliana na Tanzania kujenga bomba hadi bandari ya Tanga. Wiki iliyopita, Uganda iliandaa mikutano miwili; mmoja na maafisa wa Kenya na mwingine na maafisa wa Tanzania. Hata hivyo, maafisa wa Uganda walikataa kueleza waliyokubaliana na wenzao wa Tanzania.
Baadhi ya duru za habari zimeripoti kuwa kampuni ya Total imethibitisha kwamba itajenga bomba la mafuta kutoka Uganda hadi Tanga nchini Tanzania.