Watu kadhaa wauawa katika ghasia za uchaguzi nchini Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i51767-watu_kadhaa_wauawa_katika_ghasia_za_uchaguzi_nchini_nigeria
Asasi za kiraia na timu za waangalizi wa uchaguzi nchini Nigeria zimetangaza habari ya kuuawa makumi ya watu katika ghasia za uchaguzi mkuu uliofanyika jana Jumamosi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 24, 2019 10:52 UTC
  • Watu kadhaa wauawa katika ghasia za uchaguzi nchini Nigeria

Asasi za kiraia na timu za waangalizi wa uchaguzi nchini Nigeria zimetangaza habari ya kuuawa makumi ya watu katika ghasia za uchaguzi mkuu uliofanyika jana Jumamosi.

Clement Nwankwo, afisa wa kundi linalojiita Situation Room ambao ni mwavuli wa vyama 70 vya kiraia nchini humo amesema watu 16 wameuawa katika ghasia za uchaguzi huo katika majimbo manane ya nchi hiyo.

Nalo vuguvugu la SBM lenye makao makuu yake mjini Lagos limeripoti kuwa, idadi ya watu waliouawa katika ghasia zinazofungamana na uchaguzi huo ni 35.

Polisi ya Nigeria haijatoa taarifa yoyote kuhusiana na habari za mauaji hayo yanayoaminika kuwa na mfungamano na uchaguzi huo wa jana.

Uchaguzi huo wa jana uliandamana na miripuko katika eneo la kaskazini mashariki mwa Nigeria, ambapo baadhi ya watu hawakwenda kupiga kura mjini Maiduguri, makao makuu ya jimbo la Borno kwa kuhofia usalama wao.

Rais Buhari (kulia) na Atiku Abubakar

Haya yanajiri wakati huu ambapo  polisi ya Nigeria inaendelea kuchunguza lengo la shambulizi la wabeba silaha lililofanyika Ijumaa ya Februari 16, siku moja kabla ya uchaguzi ulioakhirishwa nchini humo na kuua watu 130. 

Matokeo ya awali ya uchaguzi wa rais unaowachuanisha vikali Rais wa sasa Muhammadu Buhari na kinara wa chama cha upinzani cha PDP, Atiku Abubakar yanatazamiwa kutolewa kufikia Jumanne ijayo.