Rais Buhari wa Nigeria kutangazwa mshindi wa uchaguzi wa urais
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i51824-rais_buhari_wa_nigeria_kutangazwa_mshindi_wa_uchaguzi_wa_urais
Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria amehifadhi kiti chake baada ya kuibuka mshindi wa uchaguzi wa urais wa Jumamosi iliyopita na kumbwaga mpinzani wake karibu kwa karibu kura milioni 4.
(last modified 2026-03-17T04:36:21+00:00 )
Feb 27, 2019 01:18 UTC
  • Rais Buhari wa Nigeria kutangazwa mshindi wa uchaguzi wa urais

Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria amehifadhi kiti chake baada ya kuibuka mshindi wa uchaguzi wa urais wa Jumamosi iliyopita na kumbwaga mpinzani wake karibu kwa karibu kura milioni 4.

Kwa mujibu wa ujumlishaji wa matokeo uliofanywa na shirika la habari la Reuters kwa kuzingatia matokeo rasmi ya Tume ya Uchaguzi, Rais Buhari mwenye umri wa miaka 76, wa chama tawala cha All Progressives Congress (APC) ameibuka mshindi wa uchaguzi wa rais kwa kuzoa kura milioni 15.2, sawa na asilimia 56 ya kura. 

Mshindani  wa karibu wa Buhari, mgombea wa upinzani Atiku Abubakar (72)  wa chama cha People's Democratic Party (PDP),  amezoa kura milioni 11.3, ambazo ni sawa na asilimia 41 ya kura kwa mujibu ya matokeo hayo.

Tume Huru ya Uchaguzi Nigeria inatazamiwa kutangaza ushindi huo wa Buhari muda wowote sasa, wa uchaguzi huo ambao ulikuwa na ushiriki wa asilimia 35.6 ya wapiga kura zaidi ya milioni 84.

Mgombea mkuu wa upinzani Atiku Abubakar

Hii ni katika hali ambayo, chama cha mgombea mkuu wa upinzani Atiku Abubakar ambaye pia aliwahi kuwa Makamu wa Rais wa Nigeria kimepinga matokeo hayo, huku kikitaka uchaguzi mpya ufanyike katika majimbo manne kati ya 36 ya nchi hiyo. 

Mwenyekiti wa chama hicho Uche Secondus hapo jana alisema matokeo yanayotangazwa hayakubaliki,  na kwamba Tume ya Uchaguzi ikishirikiana na chama cha Rais Buhari, kimechakachua matokeo ya mwisho yaliyowasilishwa katika kituo cha kitaifa cha kujumuisha matokeo.

Msemaji wa  Tume Huru ya Uchaguzi Nigeria Rotimi Oyekanmi hata hivyo anasisitiza kuwa mchakato wa uchaguzi umesimamiwa na waangalizi wa ndani na wa nje, na matokeo hayo ni halali na yanaakisi matakwa ya wapiga kura.