Ethiopia yatumia diplomasia kuzipatanisha Kenya na Somalia
Upatanishi wa Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed katika mgogoro wa mpaka wa baharini kati ya Kenya na Somalia umezaa matunda kwa kiasi fulani, baada ya nchi mbili hizo jirani kuafikiana kupunguza taharuki iliyopo kati yao.
Baada ya Abiy Ahmed kuongoza mazungumzo mjini Nairobi kati ya Rais Uhuru Kenyatta na mwenzake wa Somalia, Mohamed Abdullahi Mohamed Farmajo jana Jumatano, Ofisi ya Waziri Mkuu wa Ethiopia imesema, "Pande mbili hizo zimekubaliana kushirikiana kuelekea katika mkondo wa amani, na kuchukua hatua za kupunguza taharuki."
Mwezi uliopita, serikali ya Somalia ilikanusha madai ya serikali ya Kenya kwamba imenyakua na kupiga mnada maeneo ya mafuta yaliyopo katika mpaka unaozozaniwa kati ya nchi mbili hizo jirani na kusisitiza kuwa, haina mpango wala haikuwa na mpango wa kunadi sehemu yoyote katika eneo linalozozaniwa baharini hadi pale Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu (ICJ) itakapotatua mgogoro huo wa mpaka.
Kabla ya hapo serikali ya Nairobi ilitangaza kumrudisha nyumbani balozi wake wa Mogadishu, Luteni Jenerali Mstaafu Lucas Tumbo, ikidai kuwa uamuzi wa Somalia wa kupiga mnada eneo moja la mafuta huko mjini London nchini Uingereza ulikuwa sawa na uchokozi dhidi yake na mali yake asili.
Vilevile serikali ya Nairobi ilitangaza kumrejesha nyumbani balozi wa Somalia nchini Kenya Mohamed Nur katika kile ambacho serikali ya Kenya baadaye ilifafanua kwenye vyombo vya habari nchini humo kuwa, ni kutoa fursa kwa ajili ya majadiliano ya kila upande katika suala hilo.