Walibya waandamana mjini Tripoli kulaani hatua za Ufaransa dhidi ya nchi yao
Raia wa Libya wamefanya maandamano katika medani kuu ya mji wa Tripoli wakiwa wamevalia vizibao vya njano kama wanavyofanya washiriki wa maandamano ya vizibao vya njazo kupinga siasa za kiuchumi za serikali ya Ufaransa, ambapo nao wamelaani mienendo hasi ya serikali ya Paris dhidi ya nchi yao.
Washiriki wa maandamano hayo wamelaani vikali operesheni za Jenerali Khalifa Haftar, kiongozi wa kundi linalojiita 'Jeshi la Kitaifa la Libya' pamoja na uungaji mkono wa kijeshi wa Ufaransa dhidi ya nchi yao. Mtu mmoja katika maandamano hayo amenukuliwa akisema: "Sisi wazawa wa Tripoli kama walivyo wakazi wa miji mingine ya Libya, tumekuja hapa kuonyesha upinzani wetu kwa utawala wa mtutu wa bunduki wa Haftar na mashambulizi yake." Siku chache zilizopita, kanali ya televisheni ya Al Jazeera iliripoti kwamba, meli ndogo ya kivita ya Ufaransa ilituma silaha na zana za kijeshi kwa wapiganaji wa Khalifa haftar nchini Libya.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, boti ndogo za mwendo kasi zilitumika kupakua shehena ya silaha kutoka kwenye meli hiyo ya kivita ya Ufaransa. Aidha wiki iliyopita, Waziri wa Ulinzi wa Tunisia, Abdelkrim Zbidi alinukuliwa akisema kuwa maafisa wa usalama wa nchi hiyo waliwatia mbaroni watu 13 wakiwa na pasi za kusafiria za Ufaransa kwenye kivuko cha Ra's Ajdir katika mpaka wa Libya. Wiki iliyopita serikali ya Maridhiano ya Kitaifa nchini Libya ilitangaza kukata ushirikiano wake wa kiusalama na Paris kutokana na hatua ya Ufaransa ya kuliunga mkono kundi la wapiganaji wa Khalifa Haftar. Wapiganaji wa kundi hilo walianzisha mashambulizi makali tarehe nne ya mwezi huu dhidi ya mji wa Tripoli sambamba na kushambulia makao makuu ya serikali ya Maridhiano ya Kitaifa mjini humo. Hujuma hizo hadi sasa zimepelekea karibu watu 270 kuuawa na wengine 1300 kujeruhiwa, sambamba na watu elfu 35 kuwa wakimbizi.