UN: Somalia imepiga hatua, lakini ipambane na ugaidi na ufisadi
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema Somalia imepiga hatua kuelekea katika uundwaji wa dola thabiti, lakini bado ina kibarua cha kupambana na ugaidi, misimamo mikali ya kuchupa mipaka na ufisadi.
Antonio Guterres amesema hayo katika ripoti kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambapo amebainisha kuwa, changamoto hizo zinazoikabili Somalia hivi sasa, ni tishio kwa hatua zilizopigwa ndani ya nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
Amesema mbali na ugaidi na ufisadi, Somalia inapaswa pia kukabiliana na mgogoro wa makundi yanayobeba silaha pamoja na migogoro ya kisiasa inayotishia uthabiti wa nchi hiyo.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema kundi la kigaidi la al-Shabaab na magenge yenye mfungamano na mtandao wa al-Qaeda yangali tishio kuu kwa usalama na amani ya Somalia, na kwamba mashambulizi ya magenge hayo yamekuwa yakilenga taasisi za serikali, maafisa usalama, maafisa wa serikali na hata mikahawa na hoteli mashuhuri nchini humo.
Amesema mwezi Machi mwaka huu, mashambulizi 77 ya mabomu yalishuhudiwa nchini humo na hususan katika mji mkuu Mogadishu, idadi ya hujuma ambayo ni kubwa zaidi kuwahi kurekodiwa nchini humo ndani ya mwezi mmoja tokea mwaka 2016.
Somalia ilitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 1992 na katika miaka ya hivi hivi karibuni nchi hiyo imshuhudia kushadidi hujuma za magaidi wakufurishaji wa Al Shabab na hivyo kuwasababishia raia wa nchi hiyo matatizo makubwa.