Ripoti: Wakenya zaidi ya milioni 2 katika hatari ya kufa njaa
Mamilioni ya Wakenya wapo katika hatari ya kukumbana na baa la njaa na mgogoro mkubwa wa chakula kuanzia mwezi huu wa Julai.
Mamlaka ya Kudhibiti Ukame nchini Kenya (NDMA) imesema katika ripoti yake mpya kuwa, watu milioni 2 katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki watakabiliwa na njaa kali kutokana na ubaha wa chakula mwezi huu wa Julai.
Ripoti ya mamlaka hiyo imesema kaunti zitakazoathiriwa zaidi na uhaba mkubwa wa chakula mwezi huu ni pamoja na Turkana, Marsabit, Baringo (Pokot Mashariki), Wajir, Garissa, Tana River na Isiolo.
Mamlaka ya Kukabiliana na Kiangazi nchini Kenya imesema idadi hiyo ya milioni 2 ya Wakenya wanaokabiliwa na njaa ni kubwa mno ikilinganishwa na milioni 1.6 katika ripoti yake ya mwezi Mei mwaka huu.

Ripoti hiyo imesema iwapo hatua za dharura hazichakuliwa, hali itazidi kuwa mbaya hususan katika maeneo hayo ambayo hushuhudia kiangazi cha kiwango cha juu nchini humo.
Hii ni katika hali ambayo, mwezi Aprili mwaka huu, serikali ya Kenya ilitenga dola milioni 18.8 sawa na Shilingi bilioni 1.88 za nchi hiyo kwa ajili ya kukabiliana na baa la njaa nchini humo; sambamba na kukanusha taarifa kwamba watu kadhaa wameaga dunia kutokana na njaa katika maeno ya kaskazini magharibi mwa nchi.