Hofu ya UN kuhusu kushtadi migogoro katika majimbo ya Somalia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i54646-hofu_ya_un_kuhusu_kushtadi_migogoro_katika_majimbo_ya_somalia
Umoja wa Mataifa umeelezea wasiwasi wake kuhusu kuongezeka migogoro na mivutano baina ya majimbo yenye mamlaka ya ndani nchini Somalia kwa upande mmoja, na majimbo hayo na serikali kuu ya Mogadishu kwa upande mwingine.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 09, 2019 03:52 UTC
  • Hofu ya UN kuhusu kushtadi migogoro katika majimbo ya Somalia

Umoja wa Mataifa umeelezea wasiwasi wake kuhusu kuongezeka migogoro na mivutano baina ya majimbo yenye mamlaka ya ndani nchini Somalia kwa upande mmoja, na majimbo hayo na serikali kuu ya Mogadishu kwa upande mwingine.

Hofu hiyo imebainishwa na Mjumbe Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, James Swan ambaye hapo jana alilitembelea jimbo lenye mamlaka ya ndani la Puntland kaskazini mashariki mwa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Swan katika mazungumzo yake na Rais wa Puntland, Said Abdullahi Deni na baraza lake la mawaziri huko Garowe, ametoa mwito wa kupatiwa ufumbuzi mvutano  unaoendelea kutotoka kati ya majimbo ya Somaliland na Puntland juu ya maeneo ya Sool na Sanaag yaliyoko katika mpaka wa maeneo hayo.

Mjumbe Maalumu wa Katibu Mkuu wa UN Somalia ameeleza wasiwasi ulionao umoja huo kuhusu mapigano kwenye maeneo ya Sool na Sanaag katika miezi ya karibuni, ambayo yamefanya hali ya taharuki kuongezeka katika eneo hilo.

Eneo la Somaliland lilijitangazia uhuru wake baada ya kujitenga na Somalia1991 na kuitangaza Hargeisa kuwa mji wake mkuu. Hata hivyo hadi hivi sasa hakuna nchi yoyote duniani inayoitambua Somaliland kuwa ni nchi huru.

Huku hayo yakiarifiwa, Rais wa Somaliland, Musa Bihi amesema jitihada za eneo hilo lenye mamlaka ya ndani za kutambuliwa kimataifa kama taifa huru lenye kujitawala zimekuwa zikirejeshwa nyuma na serikali kuu ya Mogadishu na Italia.

Siku chache zilizopita, serikali ya Somalia ilikata uhusiano wake wote wa kidiplomasia na Guinea Conakry na kuituhumu nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika kuwa inaingilia masuala yake ya ndani, kutokana na hatua ya serikali ya Conakry kumpokea kwa heshima zote za rais wa nchi, Musa Bihi Abdi, Rais wa Somaliland.