Beji Caid Essebsi Rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia nchini Tunisia afariki dunia
Rais Beji Caid Essebsi wa Tunisia amefariki dunia leo akiwa na umri wa miaka 92.
Kiongozi huyo ndiye rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia nchini Tunisia ikiwa ni matunda ya vuguvugu na harakati ya wananchi katika mataifa ya Kuarabu ya kupinga udikteta. Ofisi ya Rais wa Tunisia imetangaza ramsi leo kwamba, kiongozi huyo amefariki dunia akiwa hospitalini alikokuwa akipatiwa matibabu.
Mshauri wa kwanza wa Rais wa Tunisia amesema kuwa, Rais Beji Caid Essebsi mapema asubuhi ya leo alilipelekwa hospitali ikiwa ni mara ya pili katika kipindi cha mwezi mmoja. Kiongozi huyo alifia katika hospitali ya jeshi alikokuwa akipatiwa matibabu.
Mwezi uliopita pia kiongozi huyo alilazwa katika hospitali ya jeshi mjini Tunis baada ya hali yake ya kiafya kuwa mbaya.
Beji Caid Essebsi alishinda uchaguzi huru wa kwanza nchiniTunisia mnamo 2014 kufuatia vuguvugu la maandamano katika mataifa ya Kiarabu.
Kabla ya kuwa Rais, Beji Caid Essebsi aliwahi kushika wadhifa wa Waziri Mkuu na Spika wa Bunge.
Mapema mwaka huu, Essebsi alitangaza kwamba hatogombea kiti cha urais katika uchaguzi mkuu ujao ambao umepangwa kufanyika Novemba mwaka huu.
Kwa mujibu wa Katiba ya Tunisia, Spika wa Bunge la nchi hiyo atakaimu nafasi ya Rais hadi uchaguzi mwingine utakapofanyika.