Independent: Wanawake wamepuuzwa katika mfumo mpya wa utawala Sudan
(last modified Mon, 05 Aug 2019 12:12:49 GMT )
Aug 05, 2019 12:12 UTC
  • Wanawake wa Sudan walikuwa nembo ya maandamano dhidi ya al Bashir
    Wanawake wa Sudan walikuwa nembo ya maandamano dhidi ya al Bashir

Gazeti la Independent linalochapishwa nchini Uingereza limendika kuwa, mfumo mpya wa utawala nchini Sudan umepuuza nafasi na mchango mkubwa wa wanawake katika mapinduzi yaliyouondoa madarakani utawala wa aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Omar al Bashir.

Gazeti hilo limeashia kwamba wanawake wa Sudan walikuwa fueli iliyochochea moto wa mapinduzi yaliyoiondoa madarakani serikali ya Omar al Bashir aliyeiongoza Sudan kwa kipindi cha miaka 30 na kwamba waliunda asilimia 60 hadi 70 ya waandamanaji. Limeongeza kuwa, licha ya kwamba mwanamke alikuwa nembo ya maandamano dhidi ya utawala wa al Bashir lakini wanawake hawakupewa hata nafasi moja ya uongozi katika mabaraza na taasisi zitakazosimamia serikali ya kipindi cha mpito.

Gazeti hilo limesisitiza kuwa ushiriki mkubwa wa wanawake wa Sudan katika mapinduzi ya Sudan pia ulichochewa na kupuuzwa mwanamke katika kipindi cha utawala wa Omar al Bashir ambaye aliweka sheria za kuwakandamiza.

Wanawake wa Sudan wamechangia sana katika mapinduzi dhidi ya al Bashir

Habari zinasema kuwa baadhi ya wanaharakati wa kike wa Sudan wameeleza kutoridhishwa kwao na jinsi walivyopuuzwa katika mazungumzo ya kugawana madaraka baina ya Baraza la Kijeshi lililotwaa madaraka baada ya kuondolewa madarakani serikali ya al Bashir na Muungano wa Uhuru wa mabadiliko na vilevile katika ugawaji wa vyeo na nafasi za kisaisa za utawala wa kipindi cha mpito.

Hatimaye baada ya vuta nikuvute wanajeshi na viongozi wa vyama vya upinzani nchini Sudan wametiliana saini tamko la katiba litakalowaongoza katika kuunda serikali ya mpito.

Kwa mujibu wa mapatano ya pande mbili, kipindi cha mpito kitakuwa cha miaka mitatu na miezi mitatu ambapo Baraza la Utawala litakuwa na wanachama 6 wa kiraia na 5 wa kijeshi ambao watakuwa wakiliongoza kwa zamu.

Sudan ilianza kushuhudia wimbi la maandamano ya wananchi katikati ya mwezi Disemba mwaka jana dhidi ya hali mbaya ya uchumi na kufuatia ghasia hizo jeshi la nchi hiyo tarehe 11 Aprili mwaka huu lilimpindua rais huyo wa zamani na kushika hatamu za uongozi.  

Tags